CHANZO CHA USHI‘A KUTOKA VITABU VYA SUNNI

CHANZO CHA USHI‘A KUTOKA  VITABU VYA SUNNI

Asili ya Ushi‘a ni sawa sawa na ile ya Uislamu. (Kwa maana Ushi‘a ndio Uislamu na Uislamu ndio Ushi‘a).
Tofauti kubwa iliyo baina ya Masunni na Mashi‘a ni kuhusu mshika makamu baada ya Mtume wa Uislamu. Masunni huwamini kwamba  Abu Bakar ndiye aliyekuwa mshika makamu wa kwanza; Mashi‘a  huwamini kwamba Ali ndiye mshika makamu wa haki wa kwanza.  Kama msomi asiye na chuki akichunguza matangazo ya Mtume (s.a.w.w.) kama yalivyoandikwa na Wanachuoni wa Kisunni katika  tafsir zao za Qur’ani, hadithi za Mtume (s.a.w.w.), wasifu na tarekh (historia), hana budi kukubali kwamba alikuwa ni Mtume mwenyewe ndiye muanzilishi wa Ushi‘a.
Tangazo la kwanza la kubaathiwa (Utume wa Muhammad (s.a.w.w.)) limeandamana wakati mmoja na tangazo la ukhalifa la kwanza  kutolewa kwa Ali (a.s.). 
Tukio hilo linajulikana kama “karamu ya ndugu wa karibu.” Vifungu vinavyohusu habari hii vimenukuliwa  hapa kutoka kitabu cha Tarikh cha at-Tabari: Ali (a.s.) alisema “wakati Aya ‘na uwaonye jamaa zako wa karibu’(Qur’ani 26:214),  iliposhushwa kwa Mtume wa Allah (s.a.w.w.) aliniita mimi na  akaniamrisha kutayarisha sa‘ moja (kiasi cha kilo 3) cha chakula na niwakaribishe ukoo wa  Abdu’l Muttalib ili apate kuzungumza nao. Walikuwa karibu watu arubaini, miongoni mwao walikuwepo ami zake Abu Talib, Hamza, Abbas na Abu Lahab.
Kisha Mtume wa Allah (s.a.w.w.) akatoa khutba isemayo:- ‘Enyi watoto wa Abdu’l Muttalib! Simjui mtu yeyote katika bara-Arabu yote ambaye amewaletea watu wake kitu kilicho bora zaidi kuliko kile nilichokuleteeni mimi. Nimekuleteeni mema ya hii Dunia na Akhera. Na Allah (s.w.t.) ameniamrisha nikuiteni ninyi kwake.  Ni nani basi miongoni mwenu atakayenisaidia katika jambo hili, kwa masharti  kwamba atakuwa ndugu yangu, wasii wangu na Khalifa wangu  miongoni mwenu?’”
Ali aliendelea kusema: “Hakuna hata mmoja aliyejibu; hivyo nilisema (ingawa nilikuwa mdogo kuliko wote katika umri): ‘Mimi, ewe Mtume wa Allah! nitakuwa msaidizi wako katika kazi hii.’ Basi Mtume (s.a.w.w.) akaweka mkono wake kwenye shingo yangu na kusema: ‘Hakika huyu ni ndugu yangu, wasii wangu na Khalifa wangu miongoni mwenu. Msikilizeni na mumtii.’
Waliokuwa kwenye  mkutano wote wakaamka, huku wakicheka na kumuambia Abu Talib kwamba Muhammad ameamrisha yeye kumsikiliza mtoto wake na kumtii.”

Rejea:
At-Tabari, Muhammad bin Jarir, Tarikh, Juzuu 3 (Laden: E.J.Brill, 1882- 1885) uk.1171-1173.

Ni kitu cha kushangaza kwamba katika Tarikh ya at-Tabari  toleo la Misri (Kairo) 1939 (ambao inadaiwa kuwa imechekiwa na kile cha toleo la Laden) yale maneno muhimu “wasiyyi wa Khalifati” (Wasii na Khalifa wangu)  yamebadilishwa kuwa “kadha wa kadha.”  Masikitiko yalioje kuona ulimwengu wa usomi kutoa mhanga uaminifu wake kwa ajili ya siasa.

Ni lazima itajwe hapa  kwamba hadithi hii pamoja na maneno yake imesimuliwa na wanachuoni wa Kisunni thelathini, au zaidi, Wanahistoria, Muhaddithina na Mufassirina wa Qur’ani.

Imam Ahmad bin Hanbal ameisimulia hadithi hii katika Musnad yake (Juzuu ya 1. uk.111) pamoja na sanad hii ifuatayo (1) Aswad bin Amir kutoka kwa (2) Sharik, kutoka kwa (3) al-A‘mash kutoka kwa (4) al-Minhal, kutoka kwa (5) Ibad bin Abdullah al-Asadi, kutoka kwa (6) Ali.  Sasa (1), (3) na (5) ni miongoni mwa wasimuliaji wa hadithi wa al-Bukhari na Muslim, ambapo (2) ni miongoni mwa wasimuliaji wa hadithi wa Muslim na (4) ni miongoni mwa  wale wa al-Bukhari.

Vile vile Ahmad bin Shu’ayb an-Nasa’i ambaye kitabu chake cha Sunan ni kimoja  miongoni mwa vitabu sita sahihi vya rejea vya hadithi za Masunni, amesimulia  hadithi hii kutoka kwa Ibn Abbas katika kitabu chake al-Khasa’is uk. 6. 

Kwa rejea zingine za hadithi hii, tazama al-Muraja’at cha Abdul Husayn Sharafu d-‘Din (Barua ya 20-23). 

Comments