NDOA YA IMAM ALI NA FATIMA BINT RASULILLAH (S.A.W.W)
Abul Qasim Sulaiman ibn Ahmad al-Tabrani ameandika katika Muj’am al-Kabeer hadithi ya Mtume (s.a.w.w.) iliopokewa na Abdallah bin Mas’ud kwamba amesema “Mwenyezi Mungu ameniamrisha nimwoze Fatima na Ali.”
Tabrani vile vile ameeleza hadithi ya Mtume (s.a.w.w.) iliopokewa na Jabir kwamba Mtume amesema hivi, “Watoto na dhuria wa watu wote wametokana na upande wa mwana wa kiume wao, lakini watoto wangu wanatokana na Ali”…
Yahya Amiri katika kitabu chake Riyadhul Mustatab anasema, Mtume alipokwisha mwoza Fatima na Ali akabashiri kwamba kuwaoza hawa (Fatima na Ali) ilikuwa imetengenezwa na Mwenyezi Mungu ambaye kajaalia ukoo wangu kauweka kutoka upande wa Ali.
Sheikh Abdul Haq katika kitabu chake Madarij-un- Nubuwwah ameandika hivi:- “Kati ya moja ya matokeo muhimu ya mwaka wa pili ya Hijra (2 A.H.) ni kuolewa (harusi) Fatima na Ali.”
Anas bin Malik anahadithia kwamba, “Nilikuwa kwa Mtume mara ikamdhihirikia alama ya kuteremshiwa Mtume Wahyi, nikaona na ilipokwisha tu, Mtume akasema, ‘Ewe Anas sasa hivi Jibril amekuja kwangu na ameniambia kwamba Mwenyezi Mungu anakuambia umwoze Fatima na Ali’”.
Hivyo ndoa ya Imam Ally na bi Fatumah (a.s) ni ndoa takatifu iliyopatikana kwa amri ya Allah mwenyewe ili kuandaa kizazi kitakatifu kitachochukua jukumu kubwa na zito la kuuongoza Uislamu baada ya Mtume kuaga dunia.
Watoto waliopatikana kutokana na ndoa hii ni Imam Hassan, Imam Hussein, Zainabu na Umulkuluthum (a.s). Imam Hassan ni khalifa wa pili na Imam Hussein ni khalifa watatu kwa waislamu wote kutokana na uteuzi wa Allah na kutangazwa na Mtume (s.a.w.w).
Amma wale waliojipachika ukhalifa bila kuteuliwa na Allah wala kutangazwa na Mtume, walikuwa ni viongozi wa kisekula kama viongozi wa nchi nyingi duniani leo. Lakini viongozi hasa wa waislamu ni hawa walioandaliwa na Allah.
Comments
Post a Comment