USHUHUDA WA JOSHUA CHARBONNEAU

USHUHUDA WA JOSHUA CHARBONNEAU

Joshua Charbonneau ni muislamu wa Marekani mwenye asili ya Ufaransa. Alizaliwa mwaka 1982 huko Sumter, South Carolina. Alizaliwa katika familia ya kikristo kisha akasilimu na kuwa muumini wa Kiislamu afuataye madhehebu ya Shia akiwa na umri wa miaka 17 tu. Hiyo ni baada ya kuzisoma imani, dini na madhehebu yote duniani na kugundua kuwa dini sahihi ni Uislamu pekee na madhehebu sahihi ni Ushia. 

Alipoingia Uislamu alichagua jina Mateen kwa kiarabu ambalo maana yake kwa kiswahili ni mtu imara na asiyetetereka. Yeye kama mtaalamu wa kiingereza alijifunza pia kiarabu na kubobea kabla ya kufikia miaka 26, kisha alihamia Washington DC na kujiunga na waumini wenziwe katika jiji hilo.

Amewahi kuhojiwa na Al- Anwar Hussain TV, mahojiano ambayo alipewa kichwa cha habari Safari ya kiroho, ambapo alieleza namna alivyopambana kutafuta elimu na hatimaye kuuelewa kuwa Ushia ndio Uislamu sahihih zaidi, na kujiunga nao.

Mwaka 2012 alipata wasaa wa kusafiri na timu ya television hiyo kutembelea maeneo matakatifu huko Iraq. Kuanzia mwaka 2013 amekuwa mwanachuo wa hauza chini ya usimamizi wa sheikh Mustafa Akhound iliyomo katika Imam Ali Center ya Springfield, VA.

Mateen ametengeneza vitabu kadhaa, kimojawapo kinaitwa Mateso ya Ahlulbayt na wafuasi wao (yaani Mashia) katika Historia. Kingine kinaitwa wakristo waliopambana na kuuawa kwa kuwalinda Ahlulbayt wa Mtume Muhammad (s.a.w.w)

Anasema yafuayo kama utangulizi wa kitabu chake cha wakristo waliopambana na kuuawa wakiwatetea Ahlulbayt wa Mtume Muhammad (s.a.w.w):         

Nilipofanya utafiti katika historia ya Uislamu niligundua mara nyingi kuwa wakati wa uhai wa Mtume (s.a.w.w) na pia wakati wa uongozi wa makhalifa 12 watukufu wanatokana na Mtume mwenyewe (Ahlulbayt), wakristo kadhaa walisimama kupambana dhidi ya dhulma walizokuwa wakifanyiwa Ahlulbayt wa Mtume.
                                     
Nimeshangazwa sana, kwa nini wakristo hawa walitoa maisha yao kumtetea Mtume na kizazi chake wakati wao wakiwa waumini wa dini nyingine.

Bila shaka hii imetokana na tabia za viongozi hawa ambazo zilikuwa takatifu kiasi kwamba hata waabudu masanamu, wakristo na wayahudi ambao walimchukia sana, lakini wasingeweza kupata kasoro yoyote ya kuweza kumlaumu Mtume na Ahlulbayt wake.

Hata kabla hajaanza kuutangaza Uislamu, Mtume aliitwa na makafiri kuwa ni Al-Ameen (mwaminifu) na Assadiq (mkweli). Watu hawa watukufu walichomoza mwanga wao kwa kila mtu waliyekutana nao. Tabia zao ziliwafurahisha watu na kuwashuhudisha maadili ya hali ya juu kiasi kwamba alimhudumia kila mtu kwa haki bila kujali dini yake, kabila, jinsia wala rangi yake.

Wakristo walikuwa na amani sana katika serikali ya kiislamu chini ya Uislamu wa kweli wakati wa kipindi cha Uongozi wa Mtume mwenyewe na pia kipindi kifupi cha uongozi wa Imam Ally (a.s). kipindi hiki hakuna mkristo aliyedhulumiwa kwa sababu ya dini yake.

Mtume na Ahlulbayt wake waliamini kuwa ni jukumu lao kuwasaidia watu wote kupata haki zao kwa sababu, hata kama sio waislamu bado ni wanadamu sawa na waislamu. Hivyo wanamahitaji sawa na waislamu.

Watawala (makhalifa) walinyakua madaraka baada ya kifo cha Mtume waliwatesa na kuwaua Ahlulbayt na Mashia wao kwa wingi. Tendo hili liliwaudhi sana wakristo kiasi kwamba baadhi yao walijitolea muhanga kuwatetea watukufu hawa.

Nitaandika orodha ya matukio ya kihistoria yanayoonyesha jinsi Mtume na Ahlulbayt wake walivyowatendea vyema wakristo katika zama zao. Lakini pia nitaonyesha matukio ambapo wakristo walisimama kuwatetea Ahlulbayt na wafuasi wake kutokana na dhulma za wanafiki miongoni mwa wanaojiita waislamu.

Ninapoongelea Uislamu wa kweli ninakusudia Uislamu wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) na Ahlulbayt wake na wala siongelei Uislamu wa uongo yaani ule unaotokana na watawala waliopora madaraka na kujipa vyeo vya ukhalifa na kuwatendea waislamu na wasiokuwa waislamu madhila mengi kwa madai ya kuulinda na kuusambaza Uislamu.


Maswali:
1.    Kama Mtume na Ahlulbayt wake waliwatendea wema makafiri kiasi cha kwamba makafiri waliamini kuwa Mtume ni kiongozi wao na hivyo kusimama kumtetea yeye na Ahlulbayt wake, je hawa wanaowadhalilisha na kuwachinja wanadamu (bila kujali dini zao) kwa maelfu ni wafuasi wa nani?

2.    Je nasi tunaweza kuishi vyema na watu wa imani nyingine kama alivyofanya Mtume?

3.    Hawa viongozi bandia waliopora madaraka, wanaotajwa katika habari hii ni akina nani? Wataje. 

Comments