MASUNNI WA MALIKI
WANYOOSHA MIKONO KATIKA SWALA SAWA NA MASHIA
Wafuasi wa Malik wanasema:
“Ni Sunna kuachia mikono ndani ya Sala ya faradhi.”
Na kuna kundi kubwa la
wanazuoni lililosema hivyo kabla yao, kati yao ni Abdullah bin Zubeiri, Saidi
bin Al- Musayyabu, Saidi bin Jubairi, Atau, Ibnu Jariji, An-Nakhaiy, Hasani
Al-Basriy, Ibnu Sirini na kundi la wanafiqihi. Na ndio msimamo wa Alay-thu bin
Saad, isipokuwa yeye kasema: “Isipokuwa atakaporefusha kisimamo na akawa
amechoka basi itambidi kufunga mikono.”
Na kauli iliyonukuliwa
toka kwa Imam Al-Awzaiy ni hiyari kati ya kufunga mikono au kuachia.1
Mufti wa madhehebu ya
Malik huko Ad-Dayaru Al-Hijaziya, Muhammad Abdu ameona kuwa kuachia mikono na
kufunga ni Sunna toka kwa Mtume na kuwa muumini anaporefusha kisimamo ilihali
kaachia mikono na akachoka basi anafunga mikono. Akasema kuwa kuachia mikono ni
asili na kufunga ni tawi. 2
Ama Shia Imamiyah
mashuhuri kwao ni kuwa ni haramu na hubatilisha Sala, na ni wachache sana
wamesema ni makuruhu, kama vile Al-Halbiy ndani ya Al-Kafiy 3
Uchambuzi wa rejea:
1. Hadithi ya Sahl bin
Saad. Kaipokea Bukhari.
2. Hadithi ya Wailu bin
Hajar kaipokea Muslim na kainukuu Al- Bayhaqiy kwa njia tatu.
3. Hadithi ya Abdallah
bin Mas’ud kaipokea Al-Bayhaqiy ndani ya Sunan yake na vitabu vingine.
Ufuatao ni uchambuzi wa
Hadithi ya Sahl bin Saad.
Bukhari amepokea toka
kwa Abu Hazimu toka kwa Sahl bin Saad amesema: Watu walikuwa wakiamrisha mtu
aweke mkono wa kulia juu ya dhiraa yake ya kushoto ndani ya Sala. Abu Hazimu
akasema: Silijui jambo hili, labda kama hilo litanasibishwa na Mtume.
Riwaya imebeba jukumu
la kubainisha namna ya kufunga mikono, isipokuwa baada ya njia yake ya upokezi
kukubalika tatizo linabakia kwenye hoja yake.
Wala riwaya haionyeshi
Sunna ya kufunga mikono. Hilo ni kwa vigezo viwili:
Kwanza: Laiti kama
Mtukufu Mtume angekuwa ndio muamrishaji wa kufunga mikono basi ni nini maana ya
kauli “Watu walikuwa wakiamrisha” Hivi haikuwa ni sahihi kusema Mtume alikuwa
akiamrisha? Hivi huoni kuwa hii ni dalili kuwa hukumu ya kufunga mikono ilianza
baada ya kufariki Mtukufu Mtume kiasi kwamba makhalifa na magavana wao walikuwa
wakiwaamrisha watu kufunga mikono kwa kudhania kuwa hali hiyo ndio iliyo karibu
sana na unyenyekevu?
Na kwa ajili hiyo baada
ya riwaya hiyo Bukhari akaweka mlango maalum kwa jina la mlango wa unyenyekevu.
Ibnu Hajar amesema:
“Hekima ya muundo huu (kufunga mikono) ni kuwa ni sifa ya muombaji dhalili,
nalo ni jambo linalomzuwia mtu kuchezacheza na liko karibu sana na unyenyekevu,
Bukhari alizingatia hekima hii hivyo baada yake akaleta mlango wa unyenyekevu.
Kwa ibara nyingine ni
kuwa: Kuamrisha kufunga mikono ni dalili ya kuwa watu katika zama za Mtume na
muda mfupi baada ya zama zake walikuwa wanaswali kwa kuachia mikono, kisha
baadaye ikazushwa fikra hii na hivyo wakawaamrisha watu kufunga mikono.
Pili: Hakika mwishoni
mwa njia ya upokezi kuna kitu kinachounga mkono kuwa kufunga mikono ilikuwa ni
kitendo cha waamrishaji wala si kitendo cha mwenyewe Mtukufu Mtume, kwani
amesema:
Ismaili amesema:
“Silijui jambo hili, labda kama hilo litanasibishwa kwa Mtume.” Hiyo ni kama
tutasoma kwa tamko la kutomtaja mtendaji. Maana yake itakuwa yeye hajuwi kuwa
jambo hilo ni Sunna ndani ya Sala isipokuwa linanasibishwa tu na Mtume, hivyo
riwaya aliyoipokea Sahl bin Saad itakuwa imevushwa (Yaani mlolongo mzima wa
wapokezi hadi kumfikia yeye haujatajwa).
Ibnu Hajar amesema: Na
katika istilahi za fani ya Hadithi ni kuwa mpokezi atakaposema; inanasibishwa,
Maana yake ni kuwa imevushwa toka kwa Mtume.
(Yaani mlolongo mzima
wa wapokezi hadi kumfikia yeye haujatajwa)
Haya yote ni iwapo
tutasoma kwa tamko la kutomtaja mtendaji. Ama tukisoma kwa tamko la kumtaja
mtendaji, maana yake ni kuwa Sahl ananasibisha hilo kwa Mtume.
Ibnu Hajar ndani ya
Fat’hul-Bari amesema: Ad-Daniyu
amezungumzia kuhusu kuvushwa kwa Hadithi hii akasema: Hii ina ila, kwa sababu
ni dhana toka kwa Abu Hazimu, na imesemekana kuwa laiti ingekuwa imevushwa basi
asingehitajia kusema: “Silijui jambo hili”
Uchambuzi wa hadithi Ya
Wailu Bin Hajar:
Muslim amepokea toka
kwa Wailu bin Hajar: Kuwa alimuona Mtume kainua mikono yake na kutoa takbira
pindi alipoingia kwenye Swala, kisha akajifunika kwa nguo yake, kisha akaweka
mkono wake wa kulia juu ya mkono wa kushoto. Alipotaka kurukuu akatoa mikono
yake ndani ya nguo kisha akaiinua na kutoa takbira kisha akarukuu…..
Kutumia hoja ya Hadithi
hii ni kutumia hoja ya kitendo na kitendo si hoja isipokuwa mpaka ijulikane kwa
nini katenda hivyo, na hilo ni jambo lisilojulikana. Kwa sababu dhahiri ya
Hadithi inaonyesha kuwa Mtume alikusanya pande za nguo yake akafunikia kifua
chake na akaweka mkono wa kulia juu ya mkono wa kushoto.
Je alifanya hivyo kwa
kuwa ni jambo la Sunna au alifanya hivyo ili nguo yake isifunuke bali nguo
igusane na mwili na kujikinga baridi kwa nguo hiyo?
Anuani ya kitendo
haijulikani hivyo kitendo hakiwi hoja mpaka itakapojulikana kuwa alifanya hivyo
kwa kuwa ni Sunna ndani ya Sala kufanya hivyo.
Na kuna uwezekano
mwingine nao ni kuwa kitendo cha Mtume ilikuwa ni kuzuwia nguo isifunuke ndani
ya Sala.
At-Tirmidhiy ametoa
toka kwa Abu Huraira kuwa amesema: “Mtume alikataza kufunua nguo ndani ya Sala.
Akasema: Kufunua ni mtu kuachia nguo bila kufumba pande za nguo yake mbele
yake, hivyo iwapo akiifumba hatokuwa ameifunua, na imepokewa toka kwa Mtume
kuwa ni karaha kufunua nguo ndani ya Sala.”
Hakika Mtume aliswali
pamoja na Muhajirina na Answari zaidi ya miaka kumi, hivyo laiti kama ingethibiti
kufunga mikono toka kwa Mtume basi suala hilo lingenukuliwa kwa wingi na
kuenea, na wala asingepokea Wailu peke yake huku katika kunukuu kwake kuna
uwezekano wa aina mbili.
Sura Ya Pili Ya
Hadithi:
An-Nasai na Al-Bayhaqi
wametoa ndani ya vitabu vyao kwa njia mbili tofauti toka kwa Wailu bin Hajar
amesema: “Nilimuona Mtume wa Mwenyezi Mungu anapokuwa kasimama ndani ya Swala
hufunga mkono wake wa kulia juu ya mkono wa kushoto.”
Katika tamko la
Al-Bayhaqi ni: “Anaposimama kwenye Sala hufunga mkono wake wa kushoto kwa mkono
wake wa kulia, na nilimuona Al-Qamah anafanya hivyo.”
Kutumia Hadithii kama
dalili kunategemea usahihi wa njia ya upokezi na kutimia kwa hoja.
Ama upande wa njia ya
upokezi ni kuwa japokuwa mashekhe wawili (Bukhari na Muslim) wameinukuu kwa
njia mbili tofauti lakini zote zimeshirikiana kwa kuwepo Abdallah ndani ya njia
zote mbili.
Ndani ya Sunan
An-Nasai: “Alitupa habari Abdullah”. Ndani ya Sunan Al-Bayhaqi: “Alitupa habari
Abdullah bin Jafar” na mkusudiwa ni Abdullahi bin Jafar bin Najihi Al-Saady.
Inatosha kuthibitisha
udhaifu wake kwa aliyonukuu Abdallah Ibnu Imam Ahmad toka kwa baba yake: “Wailu
alipokuwa akifika kwenye Hadithi yake humtia dosari.”
Sehemu nyingine akasema
amenukuu toka kwa baba yake toka kwa mashekhe wake kuwa alisema: “Sikuwa
naandika chochote katika Hadithi yake baada ya kunibainikia jambo lake.”
Ad-Dauriyu amesema toka
kwa Ibnu Muini kuwa: Si chochote.
Abu Hatim amesema:
Yazid ibnu Haruna aliuliza kuhusu yeye, akasema: “Msiulize kuhusu mambo.” Amr
bin Ali amesema: “Ni dhaifu.”
Abu Hatimu amesema:
Hadithi zake hukanushwa sana, anasimulia toka kwa waaminifu mambo
yasiyokubalika. Mpaka akasema: An-Nasai amesema: ‘Hadithi zake huachwa.’ Mara
nyingine akasema: “Si mwaminifu.”
Ama hoja ya Hadithi:
Kwa sababu huenda Hadithi hii ni picha nyingine ya Hadithi ya kwanza, na
tofauti ni kuwa Hadithi ya kwanza ina nyongeza isiyokuwepo kwenye Hadithi hii,
kwani katika sura ya kwanza imesemwa kuwa alijifunika nguo yake kisha akaweka
mkono
wake wa kulia juu ya
mkono wa kushoto.
Tayari imeshapita kuwa
dhahiri ya Hadithi ni kuwa Mtume alikusanya pande za nguo zake akajifunikia
kifua chake na akaweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wa kushoto ili nguo
yake isifunuke bali ibakie imegusana na mwili na ajikingie mwili wake dhidi ya
baridi.
Hivyo kwa kuwa anuani
ya kitendo haijulikani Hadithi hii haiwi hoja kwani haijulikani ni kwa nini
alifanya hivyo.
Pamoja na hayo ni kuwa
ndani ya Hadithi hii kuna ushahidi unaothibitisha kuwa kitendo cha kufunga
mikono hakikuwa kinajulikana kipindi cha mwanzo, kwa sababu ndani ya Hadithi
imekuja kauli: “Nilimuona Al-Qamah akifanya hivyo.”
Hivyo laiti kufunga
mikono ingekuwa ni jambo lililoenea kati ya maswahaba na waliokuja baada ya
maswahaba basi kusingekuwepo na kigezo cha kunasibisha kitendo hiki kilichoenea
kwa Al-Qamah mpokezi wa Hadithi toka kwa Wailu.
Na hii inaonyesha kuwa
kufunga mkono ilikuwa ni jambo lisiloenea na ndio maana Al- Qamah akalinukuu.
Sura Ya Tatu Ya Hadithi
An-Nasai ametoa kwa
njia yake toka kwa Wailu bin Hajar kuwa alisema: Nikasema: Hapana….. Kwenye
Sala ya Mtume wa Mwenyezi Mungu jinsi anavyoswali na nikamtazama. Akasimama
akatoa takbira na akainua mikono yake mpaka ikalingana na masikio yake, kisha
akaweka mkono wake wa kulia juu ya kiganja chake cha kushoto na fundo lake na muundi.
Al-Bayhaqi naye ametoa
ndani ya kitabu chake kwa tamko hilo hilo.
Kutumia riwaya hii kama
hoja kunategemea usahihi wa njia ya upokezi na hoja yake. Ama kuhusu njia ya
upokezi wa An-Nasai, ni kuwa njia hiyo imemjumuisha Aswimu bin Kulaybu Al-Kufiy.
Ibnu Hajar ametaja kuwa
alimuuliza Ibnu Shahabu kuhusu dhehebu la Kulaybu je alikuwa Mur’jia. Akasema:
Sijui, lakini Shariku bin Abdallah An-Nakhaiy amesema kuwa alikuwa Mur’jia.
Ibnu Al-Madainiy
amesema: Hawi hoja akipokea peke yake.
Ama njia ya Al-Bayhaqi
yenyewe imemjumuisha Abdallah bin Rajau. Ibnu Hajar amenukuu toka kwa Ibnu
Muini kuwa alisema: Alikuwa mwingi wa kukosea maneno, hana ubaya.
Amr bin Adiyu amesema:
si mkweli, mwingi wa kuchanganya maneno na kukosea, yeye si hoja, amefariki
mwaka 219 au 220 Hijiria.
Ibnu Hajar amenukuu
toka kwa As-Sajiy kuwa alisema ana Hadithi zisizokubalika.
Ahmad na Yahya
wametofautiana kuhusu yeye. Ahmad amesema:
Wamedai kuwa vitabu
vyake vilitoweka hivyo akawa anaandika yale aliyoyahifadhi kichwani, na ana
riwaya zisizokubalika, na wala sikusikia toka kwake isipokuwa Hadithi mbili tu.
Na maelezo kama haya kaeleza Al-Uqay’liyu toka kwa Ahmad.
Inshallah, kunako
majaliwa nitaleta ushahidi wa kuwa Mtume aliswali akiwa amefunga mikono na
hadith zilizomadhubuti kuthibitisha hilo.
Namwomba Allah atufanye
wepesi wa kuiona haki na kuifuata na pia atufanye kuwa ni wepesi wa kuuona upotofu
na kuturuzuku kuuacha.
Comments
Post a Comment