VITA VYA UHUD

VITA VYA UHUD

Katika Madarij-un-Nubuwwah imeelezwa kwamba katika vita ya Uhud maadui walipigana vita vikali vya nguvu hata Waislamu wakakimbia na wakamwacha Mtume peke yake.
Mtume kwa uchungu na ghadhabu mno iliyompata ikawa linamtoka jasho na kudondoka kutoka kipajini mwake. Kwa ghafla akamwona Ali amesimama ubavuni mwake.

Mtume akamuuliza, “Kwa nini wewe hukukimbia pamoja na wengine?” Ali akajibu, “Nikufuru (niwe kafir) baada ya kuwa nimeshaamini? Nimeahidi kukutumikia. Nina kazi gani na watoto?”
Kwa bahati mara kikundi cha makafiri (maadui) wakamwelekea mtume, hapo Mtume akamwambia Ali, “huu ni wakati wa kunisaidia na kunivusha na mashambulio ya kikundi hiki” na hakika akamtumikia kama alivyoahidi.
Ali alipopata amri hii ya Mtume aliwaangamiza maadui na idadi kubwa yao akawapeleka motoni. Wengine wote akawatawanya.
Imeeleweka kwamba siku hiyo imam Ali alipata majeraha kumi na sita (16) mwilini mwake ambayo manne katika majeraha hayo yalikuwa ya kudhuru sana, hata kila mara alipopata moja kati ya hayo alianguka kutoka farasini mpaka chini, na mara zote nne kila alipoanguka Jibril akamwinua chini, na kumweka juu ya farasi na akasema “Ee Ali pigana vizuri, Mwenyezi Mungu na Mtume wake wamefurahi nawe.”

Baadaye Jibril akamweleza Mtume namna apiganavyo Ali na ushujaa wake. Mtume akasema, “Kwa nini Ali asijitose na kujitia hatarini roho yake kwa hali yeye ni wangu na mimi ni wake?” Pale mara Jibril akasema, “Na mimi ni wenu wote wawili.”

Vile vile imehadithiwa kwamba katika vita hivyo hivyo mlinzi wa Pepo (Jannah) katika kumsifu Ali alikuwa akisema “La Saif illa Dhulfiqar Wa La Fat illa Ali Al-Karrar” (Hakuna upanga bora kuliko Dhulfiqar na wala hakuna kijana Shujaa kuliko Ali mshupavu).



Vile vile mpokea hadithi Abdul Haq katika kitabu chake hicho hicho amesema tukio la “Naadi-Aliyan Madharal Ajaib” (Mwite Ali mtoa ajabu) imetokea katika vita hivi.

Comments