ADI MWANA WA HATIM
Kabla Mtume hajaanza kuutangaza
Uislamu, waarabu walikuwa na viongozi huru wa kikabila. Watu walikuwa wamezoea
utawala wa machifu wao na walikuwa wakiwatii; na kila wakati wakiwalipa ushuru
na kodi.
Hatim, aliyekuwa mkarimu na mashuhuri
kutoka kabila la Tai alikuwa mmoja wa machifu wa kiarabu. Mwanawe ‘Adi
alimrithi baba yake baada ya kufariki kwake na kabila lake lilikubali uongozi
wake. Alikuwa akiwatoza ushuru kwa kiwango cha robo ya mapato yao kila mwaka.
Uongozi wake ulitukia sawia na
zama za Mtume (s.a.w.w). Kabila la Tai lilikuwa likiabudu masanamu, lakini Adi
mwenyewe alikuwa mkristo na aliwaficha watu wake dini yake.
Watu hao baada ya kuyafahamu
mafunzo bora ya kiislamu, walipata faraja ya kuondolewa katika mzigo wa viongozi
wao ambao mpaka wakati huo walikuwa wamelazimisha utawala wao juu ya watu. Na
watu wanaowapinga viongozi hao wa kikabila waliuawa mara moja.
Kutokana na jambo hili, Adi
kama viongozi wengine alikuwa akiutazama Uislamu kama tishio kubwa kwake na alikuwa
akificha uadui kwa Mtume (s.a.w.w) lakini uamuzi ulikuwa umeshapita. Watu
walikuwa wakiingia katika Uislamu makundi makundi na dini ya Mwenyezi Mungu
ilikuwa ikienda mbele siku baada ya siku. Alijua kwamba siku inakuja ambapo
Waislamu watakuja kumtafuta yeye pia, na huo ndio utakuwa mwisho wa uongozi
wake.
Kwa hivyo alimwamrisha
mfanyakazi wake maalum, ambaye ni mtumwa, kila siku kuwaweka tayari ngamia
wenye nguvu na mbio karibu na kambi yake na kuwa macho.
Siku moja yule mtumwa wake
alimjia na kusema “Fanya kila maandalizi unayotaka kufanya kwa sababu waislamu
wako karibu sana.” Adi alipandisha familia yake kwenye ngamia na kuchukua vitu
vilivyo kuwa na thamani na mzigo ambao angeweza kubeba na kutoroka kwenda
Damascus, ambako watu walikuwa wa dini yake.
Lakini katika kuchanganyikiwa
huko alisahau kumchukua dada yake Saffana pamoja naye na akaachwa huko nyuma.
Waislamu waliwashinda kabila
hilo kwenye vita; na baadhi yao wakachukuliwa mateka. Waislamu walimchukua
Saffana na mateka wengine na kuwapeleka Madina na kumuelezea
Mtume (s.a.w.w) kuhusu kutoroka
kwa Adi.
Wafungwa walipewa makao katika
kambi yenye ukuta mfupi karibu na msikiti. Siku moja Mtume (s.a.w.w) alipokuwa
akienda msikitini alipitia karibu na sehemu ile ya wafungwa. Saffana aliyekuwa
mwenye akili na mzungumzaji aliinuka kutoka mahali pake na kusema;
“Baba yangu amefariki na mlezi
wangu amejificha, kuwa mkarimu kwangu na Mungu atakuwa mwema kwako!!’’
Mtume (s.a.w.w) akauliza: “Ni
nani mlezi wako?” Saffana akajibu: “Adi mwana wa Hatim.”
Mtume akuliza tena: “Yule
ambaye amemtoroka Mwenyezi
Mungu na Mtume wake?”
Alipotamka maneno hayo, Mtume
(s.a.w.w) aliondoka zake. Siku iliyofuata, Saffana alirudia maneno yale yale,
na akajibiwa sawa kama alivyojibiwa siku iliyopita. Maombi yake hayakuwa na
mafanikio. Siku ya tatu alipokuwa amepoteza matumaini aliamua kukaa kimya.
Lakini kijana mmoja ambaye alikuwa akitembea nyuma ya Mtume (s.a.w.w)
alimuashiria kuwa arudie matakwa yake. Akarudia maneno yale yale.
Mtume (s.a.w.w) akasema; “Sawa
kabisa, namsubiri mtu muaminifu kutoka kwenye kabila lako. Punde tu mtu kama
huyo atakapopatikana basi nitakutuma wewe pamoja na mtu huyo kwenye kabila
lenu. Nijulishe ukipata habari za mtu kama huyo atakapokuja hapa Madina.”
Mwanamke huyo aliwauliza watu,
ni nani yule kijana ambaye alikuwa nyuma ya Mtume (s.a.w.w) aliyemhimiza
kurudia madai yake. Wakasema, alikuwa Ali.
Baada ya muda mfupi Saffana
akamjulisha Mtume (s.a.w.w) kuwa kuna watu wa kabila lake wamekuja Madina.
Mtume (s.a.w.w) akampa mavazi mapya na pesa za matumizi njiani na ngamia wa
kusafiria. Alifuatana nao moja kwa moja hadi kwa nduguye ambaye alikuwa Syria.
Wakati alipomuona nduguye,
alimkemea huku akisema; “Uliwachukua mke na watoto wako na kunisahau mimi
kumbukumbu ya baba yako!” Adi alimuomba msamaha.
Na kwa vile alikuwa ni mwanamke
mwenye hekima, Adi alimuomba ushauri kuhusu mpango wake. Alimuuliza:
“Ungenishauri nifanye nini kwa kuwa umemuona Muhammad kwa karibu? Nijiunge naye
ama nijitenge?”
“Naamini bora ungejiunga naye.
Kama yeye ni Nabii wa Mwenyezi Mungu itakuwa ni nyongeza kwenye heshima na
uungwana wako. Na kama yeye sio Mtume, anataka tu kuwa kiongozi wa kidunia,
tena kwenye sehemu (Madina), ambapo sio mbali na Yemen, hakuna mtu yeyote
atakayethubutu kukuvunjia heshima, kwa sababu ya heshima uliyokuwa nayo kwa
watu wa Yemen. Vyovyote itakavyokuwa utahakikishiwa heshima yako.”
Adi alivutiwa na wazo hilo.
Akaamua kwenda Madina na kuchunguza mwenendo wa Mtume (s.a.w.w) kwa undani.
Kama atakuwa Mtume atamfuata sawa na Waislamu wengine. Lakini ikiwa yeye ni mtu
mwenye tamaa za kidunia ya uongozi na mali, basi atashirikiana naye hadi kiasi
cha kunufaika wote sawa.
Aliingia msikiti wa Madina na
kumsalimia Mtume (s.a.w.w). Mtume (s.a.w.w) akampokea kwa heshima inayostahili
na kumkaribisha kwake nyumbani.
Walipokuwa wanaelekea nyumbani
mama mmoja aliyesawijika alishika nguo ya Mtume (s.a.w.w) na akaanza mazungumzo
naye. Muda mrefu ulipita na Mtume (s.a.w.w) alijibu maswali yake kwa upole na
subira.
Adi alijiambia moyoni, “Hii ni
ishara moja toka kwenye tabia yake kuonyesha kuwa huyu mtu ni Mtume. Watu wenye
matamanio ya kidunia hawana tabia na moyo wa kumjibu mama masikini kwa subira
kiasi hiki na upole.”
Walipoingia ndani ya nyumba,
Adi alikuta kuwa maisha yake yalikuwa ya chini sana na yasiyo na majivuno.
Palikuwa na tandiko la kulalia ambalo pia Mtume alikuwa akilitumia kwa kukalia,
lakini sasa analitandika ili Adi akalie. Adi alisisitiza kuwa Mtume (s.a.w.w)
alikalie lakini Mtume (s.a.w.w) alikataa. Kisha Adi alikalia lile tandiko na
Mtume (s.a.w.w) aliketi chini kwenye sakafu. Adi akajiwazia “Hii ni ishara ya
pili ya tabia ya huyu mtu. Hii ni tabia ya Mitume siyo ya wafalme.
Mtume (s.a.w.w) alimgeukia na
kumuuliza, “Lakini Ukristo haukuwa dini yako wewe?” Adi alijibu, “ndio, kwa
nini?” Mtume (s.a.w.w) akasema “Basi ni kwa nini na kwa misingi gani, ulikuwa
ukichukuwa robo ya mapato ya watu wako? Hiyo haikatazwi na dini yako ?”
Adi ambaye alikuwa ameficha
dini yake hata kwa watu wake wa karibu, alishangaa kusikia maneno haya kutoka
kwa Mtume (s.a.w.w). Akanena moyoni, “Hii ni ishara ya tatu kuwa mtu huyu ni
Mtume.
Kisha Mtume (s.a.w.w) alisema
“Unaona umasikini na udhaifu wa sasa wa Waislamu. Unaona Waislamu leo wanaishi
maisha ya dhiki. Wamezungukwa na makundi ya maadui na hawana usalama wa maisha
yao na mali zao. Hawana uwezo mikononi mwao. Wallahi wakati utafika karibuni
ambapo utajiri huo mkubwa utawafikia na hakutakuwa na masikini miongoni mwao.
Wallahi, maadui wao watashindwa na kutakuwa na amani kiasi cha mwanamke kusafiri
kutoka Iraq hadi Hijaz peke yake bila ya mtu kumsumbua. Wallahi, wakati
unakaribia yale makasiri meupe ya Babiloni yatakuwa katika mikono ya
Waislamu.’’
Adi aliingia katika Uislamu kwa
Imani kamili na uaminifu na alibakia kuwa mwaminifu mpaka mwisho wa maisha
yake. Aliendelea kuishi kwa miaka kadhaa baada ya Mtume (s.a.w.w). Alikuwa kila
mara akikumbuka mazungumzo yake na Mtume (s.a.w.w) wakati walipokutana kwa mara
ya kwanza na vile alivyotabiri wakati ule juu ya hali ya baadaye ya Waislamu.
Alikuwa ana mazoea ya kusema
“Wallahi katika wakati wa uhai wangu nimewaona Waislamu wakishinda na kuteka
makasiri meupe ya Babiloni, na kuna amani na utulivu kiasi cha kumwezesha
mwanamke kusafiri kutoka Iraq hadi Hijaz bila mtu kumsumbua. Wallahi naamini
siku itafika ambapo hakutakuwa na masikini miongoni mwa Waislamu.
Comments
Post a Comment