JUWAIBIR NA ZALFA
“Ingelipendeza kiasi gani lau
ungelioa au kuolewa na ukaanzisha familia, na iwe ndio mwisho wa maisha yako ya
upweke? Na hivyo ungeliweza kutimiza mahitaji yako ya kimaumbile na vile vile
yeye angelikusaidia kufikia mahitaji na malengo yako ya kidunia na ya kiroho.”
“Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu mimi
sina mali wala sura ya kupendeza, wala sijatoka kwenye ukoo wenye heshima au
nasaba. Ni nani atakayekubali kuolewa nami? Na ni mwanamke yupi apendaye kuwa
mke wa mtu masikini, mfupi, mweusi na mwenye sura mbaya kama mimi?” (Jubaibir)
“Ewe Juwaibir! Mwenyezi Mungu
alibadilisha thamani ya watu kupitia Uislamu. Watu wengi walikuwa wamepewa vyeo
kwenye jamii zilizokuwepo kabla ya Uislamu, na dini ya kiislamu ikawashusha.
Wengi walikuwa wamedharauliwa na kuonekana si chochote, na dini ya kiislamu
ikawapa heshima na hadhi kubwa na kuwainua. Uislamu umeondoa ubaguzi na ufakhari
wa kiukoo uliokuwako usio wa kiislamu.
Hivi sasa watu wote ni sawa
bila kuzingatia rangi zao na sehemu walizotoka. Hakuna yule mwenye ubora juu ya
wengine ila tu kwa kumuamini na kumcha Mwenyezi Mungu (s.w.t). Miongoni mwa
waislamu, mtu ambaye maadili na vitendo vyake ni bora zaidi kushida vyako ndiye
mbora wako. Hivi sasa fanya kama ninavyokwambia.”
Maneno haya yalizungumzwa siku
moja baina ya Mtume (s.a.w.w) na Juwaibir, wakati Mtume (s.a.w.w) alikwenda
kuwaona watu wa “Suffa.”
Juwaibir alikuwa mwenyeji wa
“Yamamah” sehemu ambayo alijulia habari za Bwana Mtume (s.a.w.w) na kuwasili
kwa dini ya Kiislamu. Yeye alikuwa ni masikini, mweusi na mfupi, lakini wakati
huo huo alikuwa ni mwerevu wakutafuta ukweli na mtu mwenye uamuzi. Alikuja
Madina ili kutazama Uislamu kwa karibu na kwa muda mfupi alisilimu na kufuata
Uislamu.
Kwa vile hakuwa na pesa, nyumba
wala marafiki, kwa kipindi fulani alikuwa akipata malazi msikitini pamoja na
Waislamu wengine masikini kwa idhini ya Mtume (s.a.w.w). Na pindi Mtume
(s.a.w.w) alipojulishwa kuwa msikiti sio sehemu ya malazi na kuishi, ilibidi
wahamishwe na kupelekwa kwingine. Mtume (s.a.w.w) alichagua sehemu nje ya msikiti
na kuwajengea kivuli. Sehemu hiyo ilijulikana kama “Suffa” na watu walioishi
hapo walitambulika kama “As-hab-u-Suffa” - wote walikuwa ni masikini kutoka
sehemu za mbali na Madina.
Siku moja Bwana Mtume (s.a.w.w)
alikuja kuwatembelea. Alipomtambua Juwaibir miongoni mwao aliamua kumtoa kwenye
maisha haya ya upweke. Wazo la kumiliki nyumba na kuwa na mke katika hali
aliyokuwa nayo Juwaibir ilikuwa ni mbali na ndoto zake. Na hiyo ilikuwa ndio
sababu ya Juwaibir kumjibu Mtume (s.a.w.w) na kwamba ingeliwezekanaje mtu
yeyote kumkubali kwa ndoa aliposhauriwa na Mtume (s.a.w.w) aowe.
Lakini ili Mtume (s.a.w.w)
kumtoa ile shaka, alimueleza mabadiliko ambayo Uislamu ulileta kwenye jamii na
kubadilisha mtizamo wa watu.
Baada ya kumtoa Juwaibir kwenye
mawazo duni, Mtume (s.a.w.w) alimuelekeza yeye Juwaibir nyumbani kwa Ziad ibni
Lubaid ili amuombe kumposa bintiye.
Ziad alikuwa ni mmoja kati ya
matajiri wakubwa wa Madina na alikuwa amehishimiwa sana na watu wa kabila lake.
Wakati Juwaibir alipoingia nyumbani kwake alizingirwa na jamaa zake na baadhi
ya watu wa kabila lake. Juwaibir aliketi na kubaki kimya kwa muda mfupi na
kisha akainua kichwa chake na kusema, “Nimewaletea ujumbe kutoka kwa Mtume
(s.a.w.w). Mngependa kuusikiza kwa siri au niuweke wazi?
Ziad alijibu, “Ujumbe kutoka
kwa Mtume (s.a.w.w) ni heshima kwangu na bora useme hadharani. Basi Juwaibir
alinena, “Mtume (s.a.w.w) amenituma nimpose binti wenu”
“Yeye ndiye aliyependekeza wazo
hilo kwa ajili yako?” aliulizwa.
“Mimi sizungumzi kwa matakwa
yangu. Kila mtu anajua kuwa mimi sio muongo”
“Hii ni ajabu! Sisi huwa
hatutoi mabinti zetu kwa watu wenye hadhi tofauti nasi wala kabila tofauti
nasi. Wewe rudi, mimi nitakwenda kuzungumza na Mtume (s.a.w.w) mwenyewe.”
Juwaibir aliondoka mahala pale
huku akinung’unika, “Wallahi, chochote ambacho Qur’ani inafunza na chochote
ambacho ndio makusudio ya utume wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni tofauti kabisa
na anachokisema Ziad.”
Wale waliokuwa karibu walisikia
manung’uniko ya Juwaibir.
Zalfa, yule binti mzuri sana wa
Ziad, aliyekuwa malikia wa urembo wa Madina, aliyasikia maneno hayo ya
Juwaibir. Alimuendea babake na kumuuliza, “Baba, ni nini huyo bwana aliyetoka
alichokuwa akisema? Na alikuwa akimaanisha nini?”
“Alikuwa amekuja kukuposa huku
akidai kuwa ametumwa na Mtume (s.a.w.w) kuhusu hilo”
“Je, haiwezekani kwamba kweli
ametumwa, na hivyo kukataa kwako kukaonyesha kutotii maagizo ya Mtume
(s.a.w.w)?”
“Wewe unaonelea vipi kuhusu
hilo?’
“Naonelea ni vyema ungemrejesha
kabla hajafika kwa Mtume (s.a.w.w), na kisha uende mwenyewe ili upate ukweli.”
Alimrejesha Jawaibir ndani ya
nyumba kwa heshima ya hali ya juu kisha yeye mwenyewe akaharakisha kwenda kwa
Mtume (s.a.w.w). Alipomuona Mtume (s.a.w.w) alisema;
“Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu,
Jawaibir amekuja nyumbani kwangu na akaja na ujumbe kama huu kutoka kwako. Mimi
ningependa kukujulisha kuwa desturi yetu ni kuwatoa mabinti wetu kwa watu wenye
hadhi sawa na yetu, tena wa kabila letu, na ambao wote ni wasaidizi na masahaba
wako.”
“Ewe Ziad, Juwaibir ni bwana
muaminifu. Hiyo hadhi na heshima ambazo wewe unazungumzia zimekwishafutwa. Kila
muumini wa kiume yuko sawa {katika madhumuni ya ndoa} kwa kila muumini wa
kike.”
Ziad alirejea nyumbani kwake na
kumuelezea jambo hilo bintiye. Kisha binti akasema, « Tafadhali usiyakatae
mapendekezo aliyotoa Mtume (s.a.w.w.). Haya maneno yananihusu mimi. Ninamkubali
Juwaibir kwa hali yake yoyote ile atakayokuwa nayo. Kama Mtume (s.a.w.w)
ameridhika nayo pia nami nimeridhia.”
Nikaha hiyo ilitimizwa
kulingana na sheria ya kiislamu. Ziad alilipa mahari kutokana na mali yake
mwenyewe na akawapa zawadi nyinginezo nzuri. Kisha walimuuliza bwana harusi,
“Je unayo nyumba ya kumpeleka biharusi?” Alisema, “Hapana, sikuwa na wazo la
kuwa nitapata mke na kuishi maisha ya ndoa naye. Bali ni Mtume (s.a.w.w) ambaye
alinijia ghafla na kuzungumza nami na kisha kunituma nyumbani kwa Ziad”
Ziad alimuandalia nyumba
iliokuwa na vyombo kamili vya matumizi ya nyumbani, na akamhamisha biharusi
huyo kwa shangwe na nderemo akiwa amepambwa kwa madoido na manukato.
Usiku ukafika, Juwaibir
hakuweza kujua nyumba iliyokusudiwa yeye ilikokuwa. Aliongozwa hadi huko na
akaingizwa kwenye chumba cha biharusi. Alipoona nyumba na vifaa vyake na
kumuangalia biharusi alivyopendeza,
alikumbuka alivyokuwa hapo awali. Kisha alijiambia,
“Nilikuwa masikini kiasi gani
wakati ninaingia kwenye mji huu. Sikuwa na chochote - siyo pesa wala uzuri,
wala nasaba yoyote wala familia. Hivi sasa Mungu amefanya utajiri wote huu kuwa
mikonini mwangu kupitia Uislamu. Kwa kweli ni Uislamu ndio umeniletea
mabadiliko haya katika muonekano wa jamii ya watu kinyume na matarajio.
Namshukuru Mwenyezi Mungu kiasi gani kwa kunipa neema ya vyote nilivyo navyo!”
Kwa upeo wa hisia za kiroho
alikwenda pembeni mwa chumba, akatumia usiku wake kwa kusoma Qur’ani na kuswali.
Kulipopambazuka ndipo akajitambua, kisha aliamua kufunga ili kumshukuru
Mwenyezi Mungu.
Wakati wanawake walipokuja
kumtembelea Zalfa asubuhi walimkuta bado hajaguswa. Walimficha Ziad jambo hilo.
Siku mbili na usiku wake zilipita hali ikiwa vilevile. Alikuwa akifunga mchana
na usiku akiswali. Wanawake wa upande wa familia ya mke wakawa na wasiwasi.
Walidhani pengine Juwaibir alikuwa hana nguvu za kiume na hakuwa na haja ya
kuwa na mke. Hatimaye walilifikisha suala hili kwa Ziad. Yeye alimjulisha Mtume
(s.a.w.w) na Mtume (s.a.w.w) alimuita Juwaibir na kumuuliza, “Je, huna haja ya
kuwa na mke?”
“Kwa bahati mbaya au nzuri,
nina haja kubwa ya kuwa naye.” “Basi kwa nini hujamkaribia bibi harusi wako?”
“Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu,
nilipoingia ndani ya nyumba ile nilijikuta kati ya neema zile. Hali ya
kushukuru na kuabudu ilinijia. Nilidhani ni bora kumshukuru Allah na kuswali
kabla ya kuchukua hatua yoyote. Usiku wa leo nitamkaribia mke wangu,
insha’allah.”
Juwaibir na Zalfa waliishi
maisha mazuri ya furaha. Wakati mwito wa vita vya Jihad (Vita tukufu)
ulipofika, alishiriki kwa roho moja kama Mwislamu shupavu, na akafa shahidi
chini ya bendera ya Uislamu.
Baada ya shahada yake, Zalfa
alikuwa ndiye mwanamke aliyetafutwa sana kwa ajili ya kuwa mke, na watu wengi
walikuwa na moyo wa kulipa mahari ya juu kabisa kwa ajili yake.
Comments
Post a Comment