MCHANGO WA NASIBA BINT KAAB
KATIKA VITA VYA UHUD
Kovu kubwa kwenye mabega ya
Nasiba, bintiye Kaab linaashiria kuwepo kwa kidonda kikubwa cha muda uliopita.
Wakati wowote wanawake, haswa vijana ambao hawakuiona enzi ya Mtume (s.a.w.w)
au walikuwa wadogo wakati huo, walipoliona shimo hilo katika bega lake,
waliuliza kwa udadisi mkubwa kuhusu tukio hilo la kutisha ambalo lilisababisha
jeraha hilo kwenye bega lake.
Walipenda kusikia kuhusu vituko
vyake vya kutisha katika vita vya Uhudi kutoka kwenye mdomo wake mwenyewe.
Nasiba hakudhani angeweza
kupigana bega kwa bega pamoja na mumewe na wanawe wawili wa kiume kwa kumlinda
Mtume (s.a.w.w) kwenye vita vya Uhudi. Alikuwa amebeba tu kiriba cha maji
mgongoni mwake ili awanyweshe majeruhi na pia alikuwa amebeba bandeji za
kienyeji kwa ajili ya kuwafunga majeraha yao. Hakuwa amejifikiria kuwa angefaa
kwa kazi yoyote nyingine siku hiyo.
Ingawa Waislamu walikuwa
wachache na walikuwa na vifaa vichache, waliweza kuwashinda vibaya maadui zao
na kuwafanya wakimbie kwenye uwanja wa vita kwa visigino vyao.
Lakini baada ya muda mfupi, kwa
sababu ya kutojali na kupuuza kwa walinzi wa “Vilima vya Ainain” maadui
walifanya shambulizi la kushitukiza kutoka nyuma yao na kugeuza ushindi wa
Waislam kuwa kushindwa. Waislamu waliokuwa wamemzunguka Mtume (s.a.w.w)
walikimbia na kumuacha Mtukufu Mtume (s.a.w.w) karibu peke yake kwenye medani
ya vita.
Nasiba alipoiona hali hiyo ya
hatari mbaya aliweka kiriba cha maji chini, na akachukua upanga mkononi mwake.
Alipigana kwa upanga na pia akatumia vizuri upinde na mishale; na akachukua
ngao iliyoachwa na mpiganaji anayekimbia.
Mara aligundua kuwa kuna adui
ambaye alikuwa akimtafuta Mtume (s.a.w.w), na akiuliza kwa sauti, “Yuko wapi
Muhammad mwenyewe?” Alimwendea ghafla na kumpiga mara kadhaa. Lakini yule mtu
alikuwa amevaa deraya mbili na hivyo mapigo yake hayakuweza kuwa na athari
kubwa mwilini mwake. Kisha akampiga yule mwanamke dhoruba kubwa kwenye bega
lake lisilo na deraya na kumjeruhi kiasi ambacho lilihitaji matibabu ya mwaka
mzima.
Alipoona damu ikimwagika kutoka
kwenye bega la Nasiba, Mtume (s.a.w.w) alimwita mmoja wa watoto wake wa kiume
ili amfunge jeraha lake. Alimfunga bandeji kwenye bega lake na akaendelea tena
kushughulika na vita.
Wakati huo huo mmoja wa watoto
wake akajeruhiwa. Mama yule alitoa bandeji na akamfunga yule kijana kwenye
jeraha lake. Mtume (s.a.w.w) akiangalia kitendo hicho na akatabasamu kwa
ushujaa na ushupavu wa bibi huyu. Baada ya mama huyo kumhudumia yule kijana
alimshauri aendelee na vita. Alipokuwa akiendelea kuzugumza maneno hayo Mtume
(s.a.w.w) alimwonyesha yule mtu ambaye alimuumiza na kumjeruhi mwanawe.
Alimshambulia yule mtu kama
simba jike na kumpiga upanga wake kwenye mguu mpaka akaanguka chini. Mtume
akasema, “Vema, sasa umelipiza kisasi. Sifa njema ni zake Mwenyezi Mungu ambaye
amekuwezesha kupata ushindi dhidi yake na kupoza jicho lako.”
Waislamu wengi walikufa
mashahidi na wengine kujeruhiwa. Nasiba mwenyewe alikuwa amejeruhiwa sana na
hakuwa na matumaini yoyote ya kuishi. Baada ya vita vya Uhud, Mtume (s.a.w.w)
aliwaamrisha wale Waislamu waliojeruhiwa kuwafuata maadui mpaka Hamra-ul Asad
ili kuhakikisha juu ya nia na hali zao.
Nasiba pia alitaka kuandamana
nao lakini yale majeraha makubwa aliyokuwa nayo hayakumruhusu kwenda.
Walipokuwa wanarudi kutoka Hamra-ul-Asad, kabla ya Mtume (s.a.w.w) kufika
nyumbani kwake, alimtuma mtu kwenda kumjulia hali Nasiba na alifurahi sana
kujua kuwa bado alikuwa hai.
Komandoo aliyefanya kazi ya
ziada ili kuulinda Ushindi wa waislamu na Uislamu wenyewe ni Imam Ally (a.s)
aliyepambana kiasi kwamba waislamu wote walikuwa wamejeruhiwa vibaya na
kushindwa kusimama isipokuwa yeye pekee. Vita hii ndio ambayo Mtume aling’olewa
meno ya mbele na kudondoshwa ndani ya Shimo na ndipo wengi wa waislamu
walidhani amekufa na kumkimbia.
Katika tukio hili sayyidna
Hamza (ra) aliuawa na waislamu waliokuwa hawana imani kamilifu kama vile
Abubakar na Umar walikimbia mbali sana na kurudi baada ya siku kadhaa.
MAFUNZO KUTOKANA NA HISTORIA
HII
1. Abubakar
na Umar hawakuwa na utukufu kama wanavyowatangaza wafuasi wao
2. Shujaa
hasa katika vita hivi ni Mtume na imam Ally
3. Mwanamke
mtukufu Nasiba alikuwa shujaa na bora kuliko wengi wa Masahaba wakiwemo
Abubakar na Umar
4. Kutokumtii
Mtume kunaleta maangamizi makubwa kwa Uislamu na waislamu.
5. Nasiba alikuwa
nesi wa kwanza kuwahudumia majeruhi vitani
Comments
Post a Comment