MWISLAMU MPYA
Majirani wawili; mmoja Mwislamu
na mwengine mkristo, walikuwa na uhusiano mzuri kama marafiki. Katika hali ile
yakujali maslahi ya kila mmojawao walikuwa wakijuliana hali, na walikuwa
wakibadilishana mawazo kila mara. Jirani Mwislamu akiwa mcha-Mungu na mwenye
kushika dini, alikuwa akiisifia sana dini yake na matokeo yake ilikuwa ni
kusilimu kwa huyo jirani Mkristo.
Usiku ulipita na ilikuwa
yakaribia alfajiri. Mkristo huyo, aliyekuwa amesilimu mara tu, alisikia mtu
akibisha mlango wake. Kwa mshangao na bila ya subira aliuliza kwa sauti: “Ni
nani wewe?
Sauti kubwa ilisikika kutoka
nyuma ya mlango, “Mimi ni fulani bin fulani,” akijitambulisha. Alikuwa ni yule
jirani Mwislamu ambaye alikuwa na heshima ya kumsilimisha kuwa Mwislamu.
“Wataka nini nyakati hizi za
usiku?”
“Harakisha, vaa nguo zako na
ushike udhu, ili twende msikitini pamoja”. Bwana huyo Mwislamu mpya, alishika udhu
kwa mara ya kwanza katika maisha yake na kuandamana na rafikiye Mwislamu hadi
msikitini. Marafiki hao walifika kabla ya wakati kuwadia. Ilikuwa wakati mzuri
wa sunna ya swala ya usiku ambayo ni baada ya usiku wa manane. Waliswali hadi
alfajiri - wakati wa swala ya asubuhi (subhi) ukaingia.
Marafiki hao waliswali swala ya
subhi, kisha wakamsabihi Mwenyezi Mungu (s.w.t) na nyuradi hadi kukapambazuka.
Wakati yule bwana aliyesilimu aliamka kutaka kuelekea mlangoni, rafiki yake
Mwislamu alimuuliza:
“Unakwenda wapi?”
“Naelekea nyumbani, maadamu
nishamaliza swala ya subhi, hakuna jambo lingine tena la kufanya sasa.”
“Subiri kiasi na umkumbuke
Mwenyezi Mungu kwa kuzitaja sifa zake (nyiradi) mpaka pale jua
litakapochomoza.” “Sawa sawa.”
Bwana huyo alikaa na kusoma nyiradi,
kama alivyoagizwa hadi jua lilipochomoza. Wakati alipoinuka ili aondoke, rafiki
yake alimpa Qur’ani mikononi na akamwambia, “Soma hadi jua lichomoze zaidi
kidogo. Na nakushauri ufunge saumu leo hii. Kwani hujui kufunga kuna ubora na
malipo (thawabu) kiasi gani?” Basi Mwislamu huyo mgeni alifuata maamrisho jinsi
alivyokuwa ameelekezwa, aliendelea kusoma Qur’ani hadi kukaribia wakati wa
adhuhuri.
Jirani Mwislamu alimwambia:
“Sasa hivi wakati wa adhuhuri umekaribia, ni bora tuswali swala ya adhuhuri
hapa msikitini.”
Hivyo swala ya dhuhri
ikaswaliwa. Kisha akasema tena: “Baada ya muda mfupi, swala ya Alasiri
itaswaliwa. Na hiyo pia inabidi tuiswali kwa wakati wake uliotengwa.” Swala
hiyo pia iliswaliwa. Kisha akasema, “Sasa hivi Magharibi imewadia” na akamuweka
aliyesilimu hadi wakati wa swala ya Magharibi.
Wakati alipoamka kufunguwa
saumu yake, jirani alimwambia, “Kuna swala moja imebaki na inaitwa “Ishaa.” Kwa
hivyo walisubiri kipindi cha swala kiingie. Baada ya hapo yule bwana aliyekuwa
amesilimu siku za karibuni aliamka na kuenda zake.
Siku ya pili yake masaa yale ya
usiku alisikia tena kubishwa hodi mlangoni. Akauliza: “Nani mwenzangu?”
“Mimi ni fulani bin fulani…..
jirani yako. Harakisha, vaa nguo zako na ushike udhuu ili tuende pamoja msikitini”
“Jana usiku baada tu ya kurudi
kutoka msikitini, nilijiuzulu na kuwachana na dini yako. Tafadhali nenda zako
na ukamtafute mtu mwingine asiyekuwa na la kufanya katika dunia hii, ili kwamba
aweze kutumia muda wake wote msikitini. Mimi ni masikini na nina mke na watoto
wa kulisha. Afadhali niendelee na shughuli zangu ili nipate riziki yangu.”
Imam Ja’far Sadiq (a.s.)
akisimulia kisa hiki kwa marafiki pamoja na wafuasi wake. Alisema, “Hivi ndivyo
yule bwana mcha Mungu baada yakumsilimisha jirani yake, yeye mwenyewe
alimfukuza kwenye Uislamu. Yabidi kila mtu azingatie jambo hili kichwani na
asiwasumbue watu bila dharura. Inawabidi mjue nguvu zao na kiwango chao na
kutenda ipasavyo, ili waweze kujenga uhusiano na dini na wasiwe ni wenye
kuikimbia. Kwani hamjui kwamba sera za Bani Ummaya zilitegemea ukatili, dhulma
na vitisho wakati ambapo njia na taratibu zetu misingi yake ni huruma, undugu
na ushawishi mzuri?”
Comments
Post a Comment