MWONGOZO

Assalaam alaykum:

Kuna njia nyingi kwa ajili ya mwanadamu kupata mwongozo na kuibuka kutoka kwenye giza na kuelekea kwenye nuru. Kwa ajili ya ustawi wa mwanadamu na ukamilifu wa maadili yake, Mwenyezi Mungu ameumba uthibitisho, ushahidi na dalili1, katika idadi kubwa kiasi kwamba ziko nje ya uwezo wa kuhesabiwa na kukokotolewa.

Kwa ajili ya mwongozo wa mwanadamu, Allah aliwatuma mitume na dalili zilizo wazi,2 vitabu, miujiza na ishara ili pengine watu wanaweza kuitambua njia iliyonyooka na kupata ustawi na mafanikio.

Katika kipindi chote cha utume wake, Mtukufu Mtume (saw), katika suala la utakatifu wa kiroho na ukamilifu wa maadili, alikuwa ni kiigizo katika kauli na matendo, na hata alisema: “Nimetumwa (kama Mtume) kwa (kusudio la) kuyakamilisha maadili.3

Tatizo la mwanadamu lipo katika kutozingatia kwake amali njema, kutenda kwake maovu, kupupia matamanio na utii kwa shetani. Baadhi ya watu wamejiachia (katika kufanya maovu) kiasi kwamba wanaendesha maisha yao kama wanyama.

Kwa lengo la utakatifu na kuyaponya madili ya wanadamu, kupunguza kasi na kudhibiti hulka ya asili, Mtukufu Mtume alifanya kila aliloliweza na alitaja yote yaliyopaswa juu ya jambo hili.

Kupata fanaka katika ulimwengu huu na ulimwengu ujao (Akhera) kunawezekana tu chini ya uangalizi wa mwalimu na wakati huo huo si kila mtu anaweza kubainisha nukta mbili za mwisho (yaani maadili bora kabisa na duni kabisa) ili kuonyesha kwa vitendo njia ya kati na iliyo sawa. Yule mwenye Hikma isiyo na kikomo aliwaleta mitume wote na hususani Mtukufu Mtume Muhammad (saw) kama “mwalimu na mkufunzi” wa maadili, ili kwa kufuata nyayo zake, watu wajitenge na maovu na wapate heshima ya duniani na Akhera.

Katika Qur’ani, kuna sura iitwayo Al-Qasas (masimulizi), ambayo yenyewe tu ni ushahidi kuwa mwanadamu anahitaji Historia na masimulizi. Ndio maana sisi Mashia tumezama sana katika Historia na tunawaomba watu wote wazame katika Historia. Wawatambue watu wema na kuwafuata na wawatambue pia waovu na kujiepusha nao.

Katika sehemu nyingi ndani ya Qur’ani, hadithi za mitume wafalme wa mataifa zimetajwa. Kwa kuongezea Mwenyezi Mungu amezungumzia masuala yanayohusiana na vita, amani, familia, dini, jamii na mada nyinginezo, katika muundo wa hadithi na masimulizi. Kwa kuvisoma visa hivi, watu wanaweza kuelewa na kutofautisha kati ya njia ya maendeleo na ile ya kuporomoka kwa maendeleo, na kupanda na kushuka katika kila kipengele, hususani maadili.

Suratul Yusuf yote imetumika kusimulia kisa cha nabii Yusuf, Yaqub, Zulekha na nduguze. Mwanzoni mwa sura Mwenyezi Mungu anasema:
“Tunakusimulia (Ewe Mtume) masimulizi bora kabisa kwa (kupitia) yale tuliyokufunulia katika Qur’an hii. (Suratul Yusuf; 12:13)
Ambapo katika aya ya mwisho sura hii, anasema katika historia yao, “kwa hakika kuna mazingatio kwa watu wenye akili.” (Suratul Yusuf 12: 111).

Kwa hakika moja ya ustadi mkubwa kabisa wa Qur’ani ni hadithi hii ya Yusuf (as) iliyotajwa kuwa ni “simulizi bora kabisa” na mwisho (Qur’ani) inasema: “katika hadithi hizi kuna mazingatio kwa wale wanaotaka kuadilika na kufuata njia ya watu watimilifu.

Juu ya hili Amirul Muuminina (as) katika Nahjul Balaghah, anamuambia mwanawe Imam Hasan (as): “Ingawa sijafikia umri ule uliofikiwa na wa kabla yangu, nimezitazama tabia zao na nimetafakari matukio ya maisha yao.
Nilitembea katika maanguko yao mpaka nikawa miongoni mwao. Kwa kweli, kwa wema wa mambo yao niliyo (bahatika) kujua, ni kama nimeishi nao mwanzo hadi mwisho.
Hivyo nimeweza kubaini kilicho kichafu na kisafi na chenye manufaa na chenye madhara.

Nimekuchagulia bora kabisa ya mambo hayo na nimekukusanyia nukta nzuri huku nikiyaacha yale yasiyo kuwa na manufaa.”

Narudia kushauri kuwa watu tusome Historia na hapo ndipo tutaweza kuchagua dini na dini, madhehebu na madhehebu, mtu na mtu, swahaba na swahaba, imam na imam. Vinginevyo tutabaki tunafitiniana kwa ushabiki tu.

Na dua yetu ya mwisho (ni) Sifa zote njema zinamstahiki Allah swt, Mola wa walimwengu.

REJEA
1. Qur’ani Tukufu, Sura Ibrahim – 14: 5
2. Ibid, Suratul Hadiid 57:25

3. Safinah al-Bihar, Juz 1,uk 411

Comments