UKARIMU

UKARIMU

Allah Mwenye Hikma, amesema:
“Kwa hakika Allah yupo pamoja na wanaojilinda na maovu na wanaofanya wema (kwa wengine).”1

Maelezao mafupi:
Allah humpenda mtu mwenye sifa ya ukarimu, kama ambavyo tu Allah ameonyesha upole kwetu, ni muhimu kwetu kuonyesha ukarimu zaidi kwa wengine. Hata kama mtu ametukosea, tunapaswa kujibu kwa upole na tusilipe uovu kwa uovu, kwani hili litaongeza mafuta kwenye moto na kuzidisha chuki na uadui.

Mwenendo wa wajumbe(na Maimamu)  wa Allah ulikuwa kwamba wakisalimiwa, wanaitikia kwa salamu iliyo bora zaidi na kwa ukamilifu zaidi na wakifanyiwa wema, walikuwa wakiulipa, (tena) kwa kuzidisha (walivyofanyiwa wao).

Wale wanaofanya wema na kuonyesha ukarimu kwa wengine, huvuta mioyo ya watu, na wakati huohuo matendo yao yanamuumiza shetani.

Lazima ikumbukwe kwamba wale wanaofanya wema huwa hawamdhalilishi (wanayemfanyia wema) au kuharibu amali zao kwa kuweka aina yoyote ya masharti (kwa huyo waliyemfanyia wema).

Myahudi masikini alipata kukutana na muabudu moto tajiri wakiwa safarini. Muabudu moto aliyekuwa anamiliki ngamia na masurufu ya kutosha kwa ajili ya safari, alimuuliza, “Ni nini imani na Itikadi yako?”

Myahudi alijibu, “Ninaamini kwamba ulimwengu huu una aliyeuumba na ninamuabudu yeye na ninaomba hifadhi kwake. Ninaonyesha wema kwa yeyote anayeikiri imani yangu, lakini
ninamwaga damu ya yeyote anayetofautiana na mimi. Ni nini itikadi yako?”

Muabudu moto alijibu, “Nina wapenda viumbe wote, simdhuru yeyote na ninaonyesha ukarimu na wema kwa marafiki na maadui pia. Mtu yeyote akinikosea, nina jibu kwa wema kwa sababu najua kuwa ulimwengu huu una muumba.”

Aliposikia hivi, Myahudi alisema, “Usidanganye sana. Mimi ni binadamu kama wewe, lakini wakati wewe unasafiri juu ya ngamia na una masurufu ya safari, hunipi chakula chako wala huniruhusu nikae kwenye ngamia wako.”

Muabudu moto aliteremka kutoka kwenye ngamia wake na akatandika kitambaa chini, akaweka chakula chake mbele ya mwenzake, myahudi alikula mkate na kisha akakaa kwenye ngamia ili kuondoa uchovu. Walikuwa wamesafari umbali fulani pamoja. Ghafla myahudi alipompiga ngamia kwa bakora alimlazimisha kukimbia. Yule Mwabudu moto alimwita:

“Ewe mtu! Nilionyesha upole kwako lakini sasa, unalipa ukarimu wangu kwa kuniacha peke yangu jangwani!”
Lakini haikujalisha chochote alichosema, nasaha zake hazikuwa na faida. “Nilikutajia kwamba nina muangamiza yeyote anaye tofautiana na mimi katika imani na itikadi,” Myahudi alimkemea huku akikimbia.

Muabudu moto alitazama juu mbinguni na kuomba: “Ewe Mola wangu! Nimemtendea mtu huyu vyema, lakini amenilipa uovu. Nitendee uadilifu.”

Alipokuwa akisema haya, aliendelea na safari yake. Alikuwa amesafiri umbali mfupi tu, ghafla macho yake yalipoangukia kwenye ngamia wake, aliyekuwa amesimama peke yake baada ya kumbwaga myahudi chini. Myahudi, aliyekuwa ameumizwa vibaya, alikuwa akilalama kwa maumivu.

Alikuwa na furaha sana, muabudu moto alichukua ngamia wake, akapanda mgongoni mwake na alipokuwa anataka kuondoka Myahudi alilalamika: “Ewe mtu rahimu! Umevuna matunda ya wema wako na nimeshuhudia matokeo ya uovu wangu; sasa kwa kuzingatia imani zako, usiondoke katika njia ya wema; kuwa mpole kwangu na usinitelekeze katika jangwa hili.”

Muabudu moto alijiwa na huruma na akamruhusu kukaa kwenye ngamia na akampeleka mjini.2

Rejea:
1. Qur’ani Tukufu Suratu’l-Nahl 16:128
2. Jawaame al–Hikayaat, uk. 24,

    Namunah- e ma’arif, Juz. 1, uk. 29

Comments