ABU AYYUB ANSAARI (sahaba mtukufu)

ABU AYYUB ANSAARI (sahaba mtukufu)
Abu Ayyub Ansaar alikuwa ni mmoja wa masahaba watukufu wa Mtukufu Mtume (saw). Mtukufu Mtume (saw) alipohama Makka kwenda Madina, makabila yote ya Madina yalimuomba akae kwao, lakini alisema:
“Sehemu nitakayokaa inategemea sehemu atakayokaa ngamia wangu.” Msafara ulipofika sehemu karibu na nyumba ya Maalik Ibn Najjar, ambayo baadaye ilikuja kuwa mlango wa msikiti wa Mtume, ngamia alikaa chini kupumzika. Lakini muda mfupi baadaye alisimama tena na akaanza kutembea, kisha akarudi sehemu ile ile aliyokuwa amekaa awali.
Watu wakaanza kumuendea Mtukufu Mtume (saw) na kumuomba akawe mgeni wao. Alipoona hivi, Abu Ayyub alinyanyua mfuko uwekwao kwenye siti ya ngamia wa Mtukufu Mtume (saw) kutoka kwenye mgongo wa ngamia na akaupeleka nyumbani kwake.
Mtukufu Mtume (saw) alipobaini kuwa mfuko wake haupo, aliuza “Nini kimetokea juu ya mfuko wangu?” Wale waliokuwepo walimjulisha kwamba Abu Ayyub alikuwa ameupeleka nyumbani kwake.
Mtukufu Mtume (saw) akasema: “Mara nyingi mtu anatakiwa aambatane na mzigo wake” kisha akaelekea kwenye nyumba ya Abu Ayyub na akakaa hapo hadi nyumba katika eneo la msikiti zilipokuwa zimejengwa.
Awali, Mtukufu Mtume (saw), alikuwa akiishi katika chumba cha chini wakati Abu Ayyub aliishi juu ghorofani lakini baadaye aliomba: “Ewe Mjumbe wa Allah! Sio sawa kwamba wewe ukae chini, wakati sisi tunaishi ghorofani juu: itafaa zaidi ikiwa utahamia juu.”
Mtukufu Mtume (saw) alikubali na akaomba vitu vyake vihamishiwe juu. Abu Ayyub alikuwa pamoja na Mtukufu Mtume (saw) na alishiriki katika vita kama Badr na Uhud, akipigana dhidi ya maadui wa Uislam akionyesha ushujaa na ukakamavu wa kusifika.
Usiku akiwa anarudi nyumbani baada ya vita vya Khaibar, Abu Ayyub alikesha usiku kucha akilinda hema la Mtukufu Mtume (saw). Asubuhi ilipopambazuka, Mtukufu Mtume (saw) aliuliza: “Ni nani yupo nje huko?”
“Ni mimi, Abu Ayyub”, lilitoka jibu.
Mtukufu Mtume (saw) alisema mara mbili, “Allah akurehemu!”
Hivyo, Abu Ayyub kwa kupitia wema wake kwa Mtume, kwa fedha zake na roho yake, alinufaika na dua hii ya Mtukufu Mtume (saw).
Rejea:
1. Bihaar al –Anwaar, Juz. 6, uk. 554
2. Payghambar Wa yaraan, Juz. 1, uk. 20-27

Comments