KUZUIWA MAJI KWA WAISLAMU
Muawiyah alikuwa akitawala
Syria kama gavana kwa muda uliokaribia miaka kumi na sita; na alikuwa akipanga
kwa siri kunyakuwa ukhalifa akitumia vizuri kila fursa iliyowezekana.
Kisingizio chake kizuri cha yeye kuasi dhidi ya Mamlaka Kuu na kutangaza ukhalifa
wake mwenyewe kilikuwa ni kuuawa kwa Khalifa Uthman.
Muawiyah hakufanya lolote
kuhusiana na maombi ya Uthman alipotaka msaada alipokuwa hai bado. Bila shaka
alikuwa akisubiri auwawe ili aweze kutumia nafasi hiyo kama kisingizio cha
mpango wake. Uthman akauwawa na Muawiya aliamua kutumia fursa ya hali hiyo kwa
lengo lake mwenyewe.
Kwa upande mwengine, watu baada
ya kuuliwa Uthman, walijikusanya nyuma ya Ali (a.s) (ambaye kwa sababu fulani
alisita kuchukua jukumu la ukhalifa) na wakatangaza kiapo chao cha utii kwake.
Ali (a.s) alipotizama na kuona jukumu hilo sasa limegeuziwa kwake rasmi,
alikubali na ukhalifa huo ukatangazwa rasmi mjini Madina, ambao ulikuwa mji
mkuu na kituo cha ulimwengu wa kiislamu enzi hizo.
Majimbo yote yaliyokuwa chini
ya utawala wa kiislamu yalikubali kumtii, isipokuwa Syria iliokuwa chini ya
uongozi wa Muawiyya. Alikataa kutoa kiapo cha utii kwa Ali (a.s). Na kumtuhumu
Ali (a.s) kuwa aliwapa hifadhi wauwaji wa Uthman. Muawiyya aliandikisha idadi
kubwa ya wapiganaji wa Syria na akajiandaa kutangaza uhuru wa jimbo lake.
Baada ya kumaliza maswala ya
vita vya Jamal (ngamia), Ali (a.s) alielekeza nadhari yake kwa Muawiyah.
Alimuandikia barua kadhaa, bila mafanikio. Pande zote mbili zilisogeza askari
kwa kukaribiana. Abul Aawar Salmi ndiye aliongoza kikosi kilichosonga mbele
upande wa Muawiyah na Malik Ashtar upande wa jeshi la Ali (a.s). Walikutana
ufukweni mwa mto
Furat.
Maelekezo yake Ali (a.s) kwa
mkuu wa jeshi lake yalikuwa kwamba wao wasiwe wa kwanza kushambulia. Lakini
Abul Aawar alifanya shambulizi kali kwa nia ya kulitia hofu jeshi la Ali (a.s).
Hapo Malik akawarudisha nyuma
kabisa wapiganaji wa jeshi la Syria. Salmi alianza kufikiria mkakati mpya.
Alikwenda hadi Ghat, mteremko kwenye ukingo wa Furati, sehemu pekee iliyokuwa
bora ya kupatia maji. Aliwasambaza warusha mikuki na mishale wake kwenye eneo
hilo na kuwazuia Malik na wanajeshi wake kukaribia sehemu hiyo.
Baada ya muda mfupi Muawiyah
aliwasili na jeshi kubwa. Muawiyah alifurahishwa sana na hatua ya mkuu wa jeshi
lake na akaamua kuongeza idadi ya wanajeshi wanaolinda eneo la njia ya kufikia
mto huo.
Wanajeshi wa Ali (a.s)
waliwekwa kwenye dhiki kutokana na upungufu wa maji. Muawiyah kwa furaha tele
alisema: “Huu ndio ushindi wetu wa kwanza.” Ila mtu mmoja tu, Amr bin Al- Aas,
waziri muerevu wa Muawiyah hakufikiria kuwa hiyo ilikuwa sera nzuri.
Kwa ule upande mwengine, Ali
(a.s) mwenyewe alikuwa amewasili na kupashwa habari kuhusiana na hali
iliyojiri. Alimtuma Saasa’a na barua kwa Muawiyah, ikimjulisha:
“Sisi tumefika hapa, lakini
vyovyote iwezekanavyo hatutaki vita vya kuuwana baina ya Waislamu. Kwa kweli
tunatarajia kusuluhisha tofauti zetu kwa mazungumzo na maelewano. Lakini
tumeshuhudia kuwa wewe na wafuasi wako mmeanza kutumia silaha za uharibifu
kabla ya kujaribu lolote. Isitoshe umewanyima maji watu wangu. Waelekeze watu
wako kuacha wafanyalo, ili tuweze kuanza mazungumzo. Bila shaka kama hamtaki
lolote ila vita sisi hatuogopi.”
Muawiyah aliposhauriana na
washauri wake, fikra ya jumla iliyokuwepo ni kutumia hiyo fursa adimu ya
kipekee na kupuuza hiyo barua.
Amr bin Al- Aas peke yake ndiye
aliyepinga fikra hiyo. Alisema, “Mnakosea, ukweli ni kwamba Ali (a.s) na watu
wake hawataki kuanza wao vita, na ndio maana wamenyamaza kimya kwa sasa na kujaribu
kuwahimiza mbadili mipangilio yenu kwa kupitia barua hii. Msidhani kuwa
watarudi nyuma kama mtapuuza barua yao na muendelee kuwanyima maji. Kwa sababu
hapo sasa watachukua silaha na hawatatosheka hadi watakapowatoa kwa fedheha
kwenye mto Furati.”
Lakini wengi wa washauri wa
Muawiyah walionelea kuwa kuwanyima maadui maji kutawadhoofisha na kuwalazimisha
kurudi nyuma. Muawiyah mwenyewe alikubaliana sana na wazo hilo. Mjadala huo
ulifika kikomo.
Sa’asa aliomba majibu;
Muawiyah, akitumia mbinu ya ucheleweshaji alimwambia kuwa atatuma majibu
baadaye. Kisha aliwaagiza wanajeshi wake wanaolinda maji yale wawe makini zaidi
na wazuie kuja na kuondoka kwa wanajeshi wa Ali (a.s).
Maendeleo haya yalimsikitisha
Ali (a.s), kwa sababu yaliondoa matumaini yote ya kumaliza hali hii kwa amani
kwa njia ya mazungumzo, na ilionyesha kuwa upande wa pili hauna nia nzuri.
Iliyobaki hivi sasa, ni kutumia mabavu. Ali (a.s) aliwahutubia wanajeshi wake
hotuba fupi nzito, iliyokuwa na madhumuni yafuatayo:
“Watu hawa wameanza dhulma na kufungua
mlango wa mgogoro na kuwakaribisha kwa uhasama. Wana njaa ya vita na wanadai
vita na umwagaji damu kutoka kwenu. Wamewanyima maji. Hivi sasa inawabidi mchague
moja kati ya hizi njia mbili, hakuna ya tatu. Ima mkubali kudhalilishwa na
kuonewa na mbaki na kiu kama mlivyo, ama mtoe kiu cha mapanga yenu kwa damu zao
chafu ili hatimaye muondoe kiu chenu na maji yale matamu. Kifo ni kuishi maisha
ya kushindwa na udhalilifu, na uhai ni kuwa mshindi hata kama ni kwa gharama ya
kifo.
Kwa hakika, Muawiyah amekusanya
idadi kubwa ya wajinga
na waliopotoka; na anatumia
vizuri fursa ya ujinga wao, hivyo kwamba wameweka shingo zao kwa shabihio la
mishale ya kifo.”
Khutba hii iliwatingisha
wanajeshi wa Ali (a.s) na kufanya damu yao ichemke. Walifanya shambulio kali
kiasi cha kuwalazimu wanajeshi wa Muawiyah kurudi nyuma na wao wakuchukua
umiliki wa sehemu ile.
Amr bin Al-Aas (ambaye utabiri
wake hivi sasa unaonekana wa kweli) alimwambia Muawiyah: “Wakati huu kama Ali
(a.s) na wanajeshi wake watakulipa na ile sarafu yako mwenyewe (vitendo vyako)
utafanyaje? Je! Waweza kuitwaa tena sehemu ile kwa mara ya pili kutoka kwao?”
Muawiyah alimuuliza, “Kwa mtazamo wako, Ali atashughulika vipi nasi sasa?”
“Naamini, Ali hatofanya kama
vile ulivyofanya wewe. Yeye hatotunyima maji. Yeye hakuja hapa kwa matendo kama
haya.”
Wanajeshi wa Ali (a.s) baada ya
kuwatoa wanajeshi wa Muawiyah kutoka sehemu ile (Ghat), walimuomba Ali (a.s)
ruhusa ya kupalinda na kuzuia maadui kuteka maji. Ali (a.s) aliwaambia,
“Msiwanyime maji. Hii ni mbinu ya wajinga. Siruhusu mikono yangu kufanya
vitendo kama hivyo. Nitakwenda kujadiliana nao kwa misingi ya Kitabu cha
Mwenyezi Mungu (s.w.t). Lau watakubaliana na mapendekezo yangu, ni vema na
kheri; na lau watakataa, nitapigana nao, lakini kiungwana na si kwa kuwanyima
maji. Sitoweza kamwe kufanya jambo kama hilo na sitawadhulumu kwa kuwawekea
upungufu wa maji.
Baada ya muda usio mrefu
baadaye wanajeshi wa Muawiyah walikuwa wakija sehemu hiyo na wakiteka maji bega
kwa bega na wanajeshi wa Ali (a.s), na hakuna yeyote aliyewazuia.
Comments
Post a Comment