SAKKAKI

SAKKAKI
Siraj al-Deen Sakkaki alikuwa ni mwanachuoni wa Kiislamu na mwenyeji wa Kharazm. Sakkaki alikuwa ni mhunzi kitaaluma.
Wakati fulani, akiwa ametengeneza boksi dogo na laini la chuma kwa jitihada kubwa na matatizo, aliamua kulipeleka kwa mfalme wa wakati huo.
Mfalme na mawaziri waliipenda kazi ile lakini wakati amesimama akisubiri ujira wake, mwanachuoni aliingia katika jumba la kifalme, ambapo kila mmoja alimheshimu na kukaa mbele yake kwa kumtukuza na heshima. Sakkaki alivutiwa sana na akauliza ni nani alikuwa. Alijulishwa kuwa alikuwa ni mmoja wa wanachuoni wa zama hizo.
Sakkaki alisononeshwa na asili ya taaluma yake na (hivyo) akaamua kutafuta elimu. Alikuwa na umri wa miaka 30 alipokwenda shuleni na kuelezea haja yake ya kupata elimu. Mwalimu wa shule alimwambia: “Katika umri wako, ninatia shaka ikiwa unaweza kupata maendeleo yoyote, nenda zako na usipoteze wakati wako bila sababu.”
Lakini baada ya kusisitiza sana, Sakkaki alipata ruhusa na kutafuta elimu. Kumbukumbu yake ilikuwa dhaifu sana, wakati fulani, mwalimu wake alimuambia ahifadhi hukumu ifuatayo ya kidini: “ngozi ya mbwa hutwaharika kwa kusindikwa;” lakini siku inayofuata alipotakiwa kuisoma mbele ya mwalimu wake, alisema: “Mbwa alisema: Ngozi ya mwalimu hutwaharika kwa kusindikwa.” Waliposikia hivi wanafunzi na mwalimu waliangua kicheko na kumkejeli.
Miaka kumi ya jitihada haikutoa matokeo yoyote kwa Sakkaki, ambaye alihuzunika na kukata tamaa. Alikwenda milimani lakini alipokuwa akitembea huko, alifika sehemu ambapo matone ya maji yalikuwa yakidondokea kwenye jiwe kutokea juu.
Udondokaji mfululizo wa maji ulikuwa umechimba shimo kwenye jiwe. Sakkaki alilichunguza jiwe kwa muda kisha akajisemea:
“Kwa hakika moyo wako sio mgumu kama mwamba huu. ukistahamili, hatimaye utafanikiwa.
Alipokuwa ameazimia juu ya hili, alirudi shuleni kwake na kuanzia katika umri wa miaka 40, alianza kusoma kwa bidii kubwa zaidi, nguvu na subira.
Sakkaki hatimaye alifikia hatua ambayo katika fani ya sarufi ya Kiarabu na fasihi, wanazuoni wa zama zake walikuwa wakimtizama kwa heshima kubwa. Aliandika kitabu Miftaah al- U’luum, ambacho kina matawi kumi na mbili ya fasihi ya kiarabu na kinaonekana kuwa ni moja ya kazi kubwa na nzuri kabisa katika somo hili.1
Rejea:
1. Dastaan-ha-e-Maa, Juz.3, uk 45

Comments