SHETANI APAMBANA NA MCHAMUNGU

SHETANI APAMBANA NA MCHAMUNGU

Katika kabila la Bani Israil, alipata kuishi mchamungu mmoja. Siku moja watu walimjulisha kuwa katika sehemu fulani, kulikuwa na mti uliokuwa ukiabudiwa na watu wa kabila hilo.

Aliposikia hivi, aliruka kwa hasira, akachukuwa shoka yake na kuondoka kwenda kuukata mti ule.
Ibilisi, akatokea mbele yake kwa sura ya mtu mzee, alimuuliza, “Unakwenda wapi?” alijibu “Nina kusudia kukata mti ambao unaabudiwa ili badala yake watu wamuabudu Allah.”

“Jizuie mpaka utakaposikia nitakayoyasema.” Ibilisi alisema kumuambia yule Mchamungu. Yule Mchamungu akamuambia aendelee kusema. Ibilisi aliendelea: “Allah ana mitume, wake kama ingekuwa ni muhimu kuuangusha mti angekuwa amewatuma kuja kufanya kazi hiyo.”

Lakini, Mchamungu hakukubaliana na Ibilisi na akaendelea na safari yake.
“Kwa vyovyote vile sitakuruhusu” ibilisi alisema kwa hasira na akaanza kupigana mieleka na mtu yule, katika mpambano huo mchamungu alimbwaga ibilisi chini.

“Subiri nina kitu cha kukuambia” alisihi ibilisi “Sikiliza! Wewe ni mtu masikini kama ungekuwa na mali ambayo kwayo ungetoa zaka kwa waumini wengine ingekuwa bora zaidi kuliko kukata mti. Ukijizuia kukata mti, nitaweka dinari mbili chini ya mto wako kila siku.”

Mchamungu akasema huku akiwaza: “Ikiwa unasema ukweli, nitatoa dinari moja kama sadaka na nitaitumia dinari nyingine.
Hili ni bora kuliko kukata mti katika hali yoyote, sijatumwa kufanya kazi hii wala mimi sio Mtume mpaka nijitwishe mzigo wa huzuni na mashaka yasiyo ya lazima.” Hivyo alikubaliana na ombi la ibilisi na akamuacha.

Kwa siku mbili, alipokea dinari mbili na akazitumia, lakini katika siku ya tatu, hapakuwa na dalili ya fedha. Akiwa ameudhika na kusononeka, akachukua shoka yake akatoka kwenda kukata ule mti.

Njiani alikabiliana na shetani, aliyemuuliza: “Unaelekea wapi?
“Ninakwenda kukata ule mti.”
“Kwa vyovyote huwezi kwenda kufanya hivyo” alisema shetani.
Kwa mara nyingine tena walianza kupambana lakini mara hii ibilisi alimzidi nguvu na akamwangusha chini, (kisha) akamuamuru, “rudi nyuma sivyo nitatenganisha kichwa na kiwiliwili chako.”

Mchamungu alisema, “Niache na nitarudi, lakini niambie ilikuwaje nikaweza kushinda katika tukio la awali?”
Ibilisi alijibu: “Katika tukio lile umetoka kwa ajili ya Allah na ulikuwa na ikhlasi katika nia yako na matokeo yake Allah akanidhoofisha kwa ajili yako, lakini safari hii ulikasirika kwa ajili ya nafsi yako mwenyewe na dinari zako na hivyo nikaweza kukuzidi nguvu.”

REJEA:
1.    Namunah-e-maarif, Juz. 1, uk. 54;
2.    Ihyaa al- uluum Juz. 4, uk.380;

3.    Riyadh al- Hikaaya, uk.140

Comments