SIRI YA MTUMWA MUAMINIFU
Sa’eed Ibn Musayyab
anasimulia: “Mwaka mmoja, kulikuwa na njaa kali na hivyo watu walikusanyika
pamoja ili kuomba dua kwa ajili ya mvua. Nilitazama hivi na macho yangu
yakamuangukia mtumwa mweusi aliyekuwa amejitenga na umati wa watu na akaibukia
kwenye kilele cha kilima kidogo.
Nilikwenda katika uelekeo
alipokuwa na nilipomkaribia, nilibaini kwamba midomo yake ilikuwa ikijongea
(akisoma) dua. Alipomaliza tu dua yake, wingu lilikusanyika angani. Alipoona
wingu, mtumwa alimsifu Allah na akaondoka. Mara tu mvua ikatupiga sana mpaka
tukafikiri kuwa tunaweza kuangamia. Nilimkimbilia mtumwa yule nikaona kwamba
ameingia katika nyumba ya Imam Sajjad (as).
Niliwasili mbele ya Imam
(as) na nikasema:
“Ewe bwana wangu! Katika
nyumba yako kuna mtumwa mweusi; tafadhali niuzie” Akasema, “Ewe Sa’eed! Kwa
nini badala yake nisikupe kama zawadi?”
Na akamuamuru mkuu wa
watumwa kuwaleta watumwa wote mbele yake. Walipokuwa wamekusanyika, nilibaini
kuwa mtumwa mweusi hakuwa miongoni mwao. Nikasema, “Ninayemtaka hayupo hapa.”
Imam (as) akasema hakuna mtumwa aliyebaki isipokuwa mmoja. Kisha akaamuru
akaletwe, mtumwa huyo alipoletwa mbele yangu niliona kuwa ndiye mtu mwenyewe
niliyekuwa nikimtafuta na hivyo nikasema: “Huyu ndiye ninayemhitaji!”
“Ewe mtumwa! Kuanzia sasa,
Sa’eed ni bwana wako na nenda naye” aliagiza Imam (as). Mtumwa akanigeukia na
kusema, “Ni nini kilichokusukuma unitenganishe na bwana wangu?” Nikajibu,
“Niliposhuhudia dua yako ya mvua ikijibiwa nilitamani kukumiliki.” Aliposikia
hivi, mtumwa alinyoosha mikono yake kwa ajili ya dua na akigeuzia uso wake
angani akiomba: “Ewe Mola wangu! Hii ilikuwa ni siri baina yangu na wewe. Sasa
kwa vile umeivujisha, nipatie kifo na unichukue kwako.”
Imam (as) na wote waliokuwepo
walibubujikwa na machozi kutokana na hali ya mtumwa, huku nikitokwa na machozi
nilitoka nje ya nyumba. Nilipofika nyumbani kwangu tu, mjumbe wa Imam (as)
alifika na kusema, “Njoo kama unataka kushiriki katika mazishi ya sahibu yako.”
Nilirudi nyumbani kwa Imam (as) pamoja na yule mjumbe na kukuta mtumwa
ameshafariki.
REJEA:
Muntahal Aamal, Juz. 2, uk.
38;
Ithbaat al- Wasiyyah (cha
Maasudi)
Comments
Post a Comment