HOJA YA 1 YA WAPINGA MAULID
Wanadai kuwa maulidi hayakuwako zama za Mtume Muhammad (s.a.w.w.) Kwa
hivyo, kuyaleta baada ya yeye kufariki dunia, ni bid'a (uzushi). Na kila bid'a,
kwa maneno yake mwenyewe Bwana Mtume (s.a.w.w.), ni upotevu. Kwa hivyo, kila anayesoma
maulidi amepotea!
MAJIBU YETU: Ni kweli kwamba maulidi, hivi
tunavyoyasoma, hayakuwako zama za Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Lakini si kweli kwamba, kulifanya kila ambalo halikuwako zama hizo, ni
upotevu. Kama ni hivyo, basi bila shaka Waislamu wote leo -- wakiwamo wanaopinga maulidi -- wangelikuwa wamepotea
kwa kuwa (katika zama zao mbalimbali) wamefanya, na wanaendelea kufanya, mambo
ambayo hayakuwako zama za Bwana Mtume (s.a.w.w.)!
Kwa mfano, katika zama za Bwana Mtume (s.a.w.w.), misikiti haikuwa
ikitandikwa chochote (watu wakisujudu juu ya mchanga); lakini leo inatandikwa
majamvi, busati na mazulia! Kiwanja kitakatifu cha Al-Kaaba kilikuwa ni mchanga
mtupu na mawe; lakini leo kimetandikwa marumaru! Watu walikuwa wakenda kuhiji
kwa kupanda ngamia au majahazi; lakini leo wanakwenda kwa ndege, meli za kisasa
na mabasi ya anasa (luxury)!
Watu, walipokuwa wengi msikitini, lakini walikikhutubu kwa kupaza sauti
zao; lakini leo wanatumia vipaza sauti (loud
speakers)! Misahafu ilikiandikwa kwa mkono, juu ya ngozi na mifupa, na
kutolewa nakala chache; lakini leo inachapwa kwa mashini, juu ya karatasi za
fakhari, na kutolewa nakala mamilioni kwa mamilioni!
Lakini hakuna anayesema -- hata hao wanaopinga maulidi hawasemi --
kwamba Waislamu waliobuni mambo hayo wametuletea bid'a au wamepotea. Kwa nini? Kwa sababu kwao wao, na kwa wanaosoma
maulidi, uzushi wa aina hiyo si bid'a;
sio alioukusudia Bwana Mtume (s.a.w.w.). Alioukusudia yeye ni ule wa kuzua
jambo katika dini hii ambalo halitokani nayo (maa laysa minhu). Hilo
ndilo lililo wazi kutokana na Hadithi mashuhuri ya Bwana Mtume (s.a.w.w.)
inayosema: "Yeyote atakayezua, katika dini
yetu hii, jambo ambalo halitokani
nayo, litarudishwa (litakataliwa)."
Ukiitaamali vizuri Hadithi hiyo, itakudhihirikia kwamba Bwana Mtume
(s.a.w.w.) hakutuzuia kuzua (kubuni),
katika dini hii, kila ambalo
halikuwako zama zake. Kama angelitaka kutuzuia hivyo, Hadithi hiyo isingelisema
hivyo, bali ingelisema hivi: "Yeyoye atakayezua jambo katika dini yetu
hii, litakataliwa." Na lau ingelisema hivyo, basi yote yale tuliyoyataja
hapo juu yasingeliruhusiwa; yangelikuwa bid'a.
Lakini Hadithi haikusema hivyo. Ilivyosema ni:
"Yeyote atakayezua … ambalo
halitokani nayo, litakataliwa." Kwa kuongeza kifungu cha maneno
tulichokichapa kwa italiki (yaani
"ambalo halitokani nayo"), ni wazi kwamba Mtume Muhammad (s.a.w.w.)
hakukusudia kuwazuia Waislamu kufanya kila
ambalo halikuwako zama zake. Alilolikusudia ni kutuachia wazi mlango wa
kubuni mambo katika dini hii bora tu yawe
yanatokana nayo.
Sasa suali hapa ni: jee, maulidi si katika mambo yanayotokana na
"dini hii", hata kama hayakuwako zama za Bwana Mtume (s.a.w.w.)?
Majibu yetu ni: Maulidi, na yaliyomo maulidini, si mageni na "dini
hii", bali yanatokana nayo, kama tutakavyobainisha kwa urefu zaidi katika
majibu yetu baadaye insha Allah.
Kwa hivyo, kuwa tu jambo halikuwako zama za Mtume Muhammad (s.a.w.w.)
si hoja ya kuwazuia Waislamu kulifanya. Wanalozuiliwa Waislamu kulifanya ni kuzua jambo na kulifanya ni dini hali ya
kuwa halina asili na dini. Na maulidi si hivyo!
Comments
Post a Comment