HOJA YA 2 YA WAPINGA MAULID

HOJA YA 2 YA WAPINGA MAULID

Wanadai kuwa Maulidi hayakusomwa na maswahaba wala waandamizi wao (taabi'in). Kama kweli yangelikuwa ni sawa kuyasoma, bila shaka mabwana wakubwa hao wangelikuwa ni wa mbele kufanya hivyo.

MAJIBU YETU: Hakuna Mwislamu yoyote anayekataa kuwa maswahaba ni watu watukufu. Wala hakuna anayekataa kuwa wao ndio kiungo chetu sisi na Bwana Mtume (s.a.w.w.). Lakini, pamoja na utukufu wote huo, wao walikuwa ni binadamu; hawakuwa ni ma'asumin. Walikiweza kufanya jambo, wakaswibu (wakapata); kama ambavyo walikiweza kufanya jambo, wakakosea. Na mifano ya yote mawili hayo ni mingi katika historia yao.

Kwa hivyo, kuwa tu jambo fulani halikufanywa na maswahaba, haliwi ni hoja sahihi ya kuwazuilia Waislamu kulifanya jambo hilo. Hoja ya pekee iliyo sahihi ni iwapo lile ambalo hawakulifanya wao, waliacha kulifanya kwa sababu ndivyo alivyoamrisha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w.), au waliacha kulifanya kwa sababu linapingana na maamrisho ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w.). Ikiwa walifanya hivyo ndipo jambo hilo litakapokuwa ni hoja; lakini si kwa sababu ya kuwa halikufanywa na maswahaba, bali ni kwa sababu tu ya kuwa ndivyo alivyoamrisha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w.), au ni kwa sababu tu ya kuwa linapingana na mafunzo ya Mwenyezi Mungu na Mtume Wake (s.a.w.w.) -- na hivyo ndivyo Kiislamu.

Kwa hivyo si sawa kuyapinga maulidi kwa sababu tu hayakusomwa na maswahaba na waandamizi wao. La sawa ni kuyapinga kwa sababu tu yamekatazwa na Mwenyezi Mungu au Mtume Wake (s.a.w.w.), au yanapingana na maamrisho yao. Na hilo, mpaka hivi sasa, wapinzani wa maulidi hawajaweza kulithubutisha.

Tunasema hivyo kwa sababu, mmoja kati ya misingi muhimu ya sharia ya Kiislamu, inayokubaliwa na wanazuoni wa wanaosoma maulidi na wale wa wanaopinga maulidi, ni kwamba -- tunapokuja kwenye mambo kama ya maulidi, ujenzi wa msikiti, mavazi, na kadhaalika -- kila kitu ni halali mpaka kithibitishwe kuwa ni haramu. Kwa hivyo, kwa msingi huu, uharamu wa maulidi haitaki uthibitishwe na wanaoyasoma, bali inataka uthibitishwe na wanaoyapinga. Wala wasilithibitishe hilo kwa vichwa vyao (Sura 16:116), bali kwa kutoa ushahidi wa maneno ya Mwenyezi Mungu au Mtume Wake s.a.w.w. (Sura 4:59). Na hilo pia, mpaka dakika hii, wapinzani wa maulidi hawajaweza kulifanya.

Mwanzo mwanzo wa kuzuka madhihabi haya ya kupinga maulidi, wafuasi wake waliyapinga mambo mengi yaliyozuka katika zama zao. Kati ya mambo hayo ni kuvuta sigara, kupiga simu ya waya (telephone), kujiwekea kashida mbele ya mtu anaposwali, kumwamkia mtu kuwa: "Umeamkaje?", kupana mikono baada ya swala, kutandika busati misikitini, na hata kuvaa nguo yenye thamani inayozidi dirhamu 100 (mia)!

Yote hayo waliyapinga kwa hoja ya kuwa hayakuwako zama za Mtume (s.a.w.w.), na kwamba hayakufanywa na maswahaba na waandamizi wao! Lakini, baada ya kutambua walikosea wapi, walirudi nyuma, wakayakubali yote hayo. Kwa maneno mengine, yakawa sio bid'a tena!

Leo, kwa hoja hizo hizo, waandamizi wao wameanza kusema vibula vivunjwe! Kesho watasema na minara nayo ivunjwe! Kesho kutwa watasema mimbari za mbao au za mawe, nazo pia ziondolewe, zirudishwe zile za vigogo vya mtende; hata vya mnazi havitafaa! Baada ya hapo ni nini kitakachowazuia wasitwambie tuondoe feni misikitini, turudi kujipepea kwa nguo zetu kama ilivyokuwa zama za Bwana Mtume (s.a.w.w.)? Au twende hijja kwa ngamia au farasi badala ya ndege? Au ni lipi litakalowazuia kutuamrisha kuisoma Qur'ani katika ngozi na mbao, kama ilivyokuwa zama za Bwana Mtume (s.a.w.w.) na maswahaba, badala ya hii miswahafu mizuri mizuri tuliyonayo?

Ni matumaini yetu kwamba, kama ambavyo watangulizi wao walirudi nyuma na kuyakubali yale waliyoyafanya ni bid'a mwanzo, wao nao watafuata nyayo zao, wayaone maulidi, na mengine kama maulidi, kuwa sio bid'a iliyokatazwa na Mtume Muhammad (s.a.w.w.). Alhamdulillaah, baadhi yao wameanza kuona hivyo na kufanya sherehe za mazazi ya Bwana Mtume (s.a.w.w.). Lakini badala ya kuyaita maulidi, huyaita seera (huu ni ujanza wa kitoto wa kubadili jina, kwa kitu kilekile wakipingacho)! 

Comments