HOJA YA 3 YA WAPINGA MAULID
Wanadai kuwa kuweka ada ya kusoma maulidi ni kuigiza Wakristo walioweka
siku ya Krismasi; na Mwislamu haruhusiwi kufanya hivyo.
MAJIBU YETU: Mwislamu
hazuiliwi kufanya jambo kwa sababu tu
linafanywa na Mkristo au kafiri yeyote mwengine. Analozuiwa ni kufanya jambo
kama linalofanywa na Mkristo, au kafiri, linapokuwa linakwenda kinyume na
mafunzo ya Kiislamu; na hilo sio linapofanywa na Mkristo au kafiri yeyote tu,
bali hata linapofanywa na Mwislamu mwenziwe; haruhusiwi kulifanya.
Tunaposoma historia, kwa mfano, tunaona jinsi Bwana Mtume (s.a.w.w.) --
katika Vita vya Handaki -- alivyokubali shauri la Salman Farsi la kuchimba
handaki kama walivyokifanya Wafursi kwao. Na Wafursi, wakati huo, hawakuwa ni
Waislamu, bali walikuwa ni makafiri waliokiabudu moto! Jee, kwa kuwaigiza
makafiri hao katika uchimbaji wa handaki, Bwana Mtume (s.a.w.w.) alikosea?
Hali kadhaalika, tukija kwenye hijja mathalan, tunaona jinsi mahujaji
wanavyokwenda baina ya Swafaa na Marwa, na jinsi wanavyochinja wanyama mwisho
wa hijja yao. Lakini vitendo kama hivyo, kabla ya Uislamu, vilikuwa vikifanywa
na makafiri! Basi kama kuigiza Wakristo hakuruhusiwi, kwa nini Mwenyezi Mungu
na Mtume Wake (s.a.w.w.) wakatuamrisha kufanya mambo ambayo dhahiri yake ni
sawa na kuwaigiza makafiri?
Ukivizingatia vizuri vitendo hivyo utaona kwamba, japokuwa kwa dhahiri
vinafanana na vile vya makafiri, kwa kweli huwezi kusema kuwa ni sawa na
kuwaigiza makafiri. Kwa nini? Kwa sababu waliyokuwa wakiyafanya makafiri mahali
humo, walikuwa wakiyafanyia masanamu yao, waliyoyaweka humo. Kwa hivyo yao
ilikuwa ni shirk (ushirikina). Lakini
tunayoyafanya sisi Waislamu, baada ya kuondolewa mbali masanamu hayo, huwa
tunamfanyia Mwenyezi Mungu Mmoja tu, asiye na mwenziwe (mshirika). Kwa hivyo
yetu ni tawhid (kumpwekesha Mwenyezi
Mungu).
Hali kadhaalika tunapokuja kwenye Krismasi. Japokuwa Krismasi, kama
maulidi, hufanywa kwa kusherehekea mazazi ya Mitume ya Mwenyezi Mungu (Nabii
Muhammad s.a.w.w. na Nabii Isa a.s.), lakini sherehe mbili hizo -- kama ambavyo
kila mtu anajua -- si sawa. Sherehe zinazofanywa Krismasi ni tafauti kabisa na
zinazofanywa maulidini, kama ambavyo Wakristo wanavyomchukulia Nabii Isa a.s.
(Yesu Kristo) ni tafauti kabisa na vile Waislamu wanavyomchukulia Mtume
Muhammad (s.a.w.w.). Kwa mfano, Waislamu hawamchukulii Mtume Muhammad
(s.a.w.w.) kuwa ni Mungu, wala ni Mtoto wa Mungu, wala ni Roho Mtakatifu.
Kwa hivyo kuwa tu jambo
fulani lilitangulia kufanywa na makafiri -- wawe ni Wakristo ama ni wengineo --
haiwi ni hoja ya kuwazuilia Waislamu
kulifanya jambo hilo maadamu watayatoa
yote ya ukafiri yaliyokuwamo humo. Na hivyo ndivyo maulidi yalivyo. Zaidi ya
kuwa zote mbili -- Krismasi na maulidi -- ni sherehe za mazazi ya Mitume wa
Mwenyezi Mungu, hakuna jingine linalofanana katika sherehe hizo.
Kama tutashikilia kuwa ni haramu Waislamu kuwaigiza Wakristo, au
makafiri wowote kwa jumla, katika jambo lolote -- hata kama halipingani na dini
yetu -- basi sio wanaosoma maulidi tu, bali hata wanaoyapinga pia watakuwa
makosani. Kwani ni nani kati yao aliyeacha gari au ndege, akaendelea kupanda
punda, farasi au ngamia? Ni nani, anayejimudu, aliyeacha kutumia umeme,
akaendelea na kuni au mafuta ya taa? Ni nani anayeradhiwa kujipepea kwa kipepeo
au nguo yake, akaacha -- ikiwa anayo nafasi -- kutumia feni au AC (Air Conditioner)? Ni nani anayepanda
kwa miguu mpaka ghorofa ya 15, au ya 10, akaacha lifti? Kwa nini hawayaachi
yote hayo ili wasiwe wanawaigiza Wakristo au makafiri wengine, maana yote hayo
yameanzishwa na wao.
Kwa hivyo si sawa kuwazuilia
Waislamu kusoma maulidi kwa sababu tu
ya kuwa, kufanya hivyo, ni kuwaigiza Wakristo katika sherehe zao za Krismasi.
Comments
Post a Comment