HOJA YA 4 YA WAPINGA MAULID
Wanasema kuwa Kwenye sherehe za maulidi hufanywa baadhi ya mambo ambayo
ni ya munkar (yanayochukiza, bali ni
haramu kamwe, katika sharia ya Kiislamu).
MAJIBU YETU: Hiyo si hoja
madhubuti. Kwa nini maulidi yote
yatupwe kwa sababu tu ya kufanywa baadhi ya mambo ambayo ni ya munkar
katika sherehe zake? Kwa nini hayaondolewi hayo ya munkar, kama yako,
yakabakishwa yasiyo ya munkar? Kwani tunda likiwa limeoza kidogo hutupwa lote,
au hukatwa pale palipooza likaliwa pale pazuri palipobaki?
Katika hili tuna funzo zuri kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Yeye aliondoa
tawafu ya Al-Kaaba, na Swafaa na Marwa, kwa sababu mwahali humo mulikuwa na munkar (masanamu) au aliamrisha
yaondolewe hayo masanamu na watu waendelee kutufu? Tutaona kuwa Mwenyezi Mungu
hakutuzuia kufanya jambo zuri lililokuwako (kutufu na kusa'yi) kwa sababu tu katika ibada hizo palikuwa
na munkar (masanamu). Alilolifanya ni
kuondoa munkar uliokuwako, akatuacha
tuendelee na mazuri yaliyobaki (tawafu).
Kwa hivyo, kama katika maulidi kuna munkar
wowote, la sawa ni uondolewe munkar
huo, na maulidi yaachwe yaendelee. Si kumtupa jongoo na ung'ongo (ujiti) wake.
Comments
Post a Comment