SHEREHE ZA MAULIDI

SHEREHE ZA MAULIDI
Maulidi ni Kiswahili cha neno la Kiarabu, mawlid. Neno hili lina maana ya "mazazi" au "kuzaliwa kwa…" (birthday). Kwa kawaida, linapotumiwa na Waislamu, huwa na maana ya siku aliyozaliwa Mtume Muhammad (s.a.w.w.), au hafla ya kuisherehekea siku hiyo.
Waislamu wa ulimwengu mzima, ifikapo tarehe 12 ya Mfungo Sita (Rabiul Awwal), husoma maulidi na kuisherehekea siku hiyo kwa furaha kubwa. Sherehe hizo, kwa desturi, haziishii tarehe hiyo tu, bali huendelea hata kwa miezi miwili mitatu baada ya hapo. Hili huwa ni kwa sababu ya Waislamu wa kila nyumba, kila mtaa, kila mji na kila nchi kutaka kushiriki katika sherehe hizo na kupata baraka zake.
Vile vile huwapa Waislamu nafasi ya kutembeleana na kushirikiana katika sherehe hizo - jambo ambalo lisingewezekana lau watu wote wangeliamua kuzifanya sherehe hizo siku hiyo hiyo moja tu.
Waislamu wote kwa madhehebu yote husherehekea sana siku ya kuzaliwa Mtume wetu.
Wapingao maulid ni kikundi kidogo kilichofundishwa imani potofu na Muhammad Abdulwahhabi na masheikh wenzake waliopewa mishahara minono na serikali ya Uingereza ili kuzua migogoro baina ya waislamu na kuwazuia waislamu kuitangaza dini yao kwa ukamilifu. Wengi wa waislamu wa sasa asili ya kusilimu kwao ni kwa kusikiliza mawaidha na sifa za Mtume zilizokuwa zikitolewa kwenye Maulid.
Ninakuombeni waislamu wenzangu tuendeleze ibada hii muhimu ambayo inaambatana na tabligh na utoaji wa sadaka. Ibada hii inasaidia kuuinua Uislamu na kuutangaza ndani ya jamii zetu.

Comments