HADITHI SAHIHI ZA KUNYOOSHA (AU KUACHIA) MIKONO KATIKA SWALA (KWA MUJIBU WA SUNNI)

HADITHI SAHIHI ZA KUNYOOSHA (AU KUACHIA) MIKONO KATIKA SWALA (KWA MUJIBU WA SUNNI)
Hadithi ya Abu Humeid As-saidiyyu:
Hadithi hii ya Humeid As-saidiyyu, imepokelewa na Wanahadithi wengi, bahthi itakuwa ndevu sana ikiwa tutataja kila mtu alivyoipokea, lakini ngoja tuitaje kwa mujibu wa maelezo ya Bayhaqiy. Bayhaqiy amesema: Ametupa habari Abu Abdillah Al-Haafidhu: Akasema: Akasema Abu Humeidi As-saidiyyu:
"Mimi ni Mjuzi zaidi wa swala ya Mtume (s.a.w.w)" .Wakasema: Kwa nini? Ilhali haukumfuata mara nyingi zaidi yetu na wala hukutangulia kuwa naye kabla yetu?!" Akasema, 'Ndio', wakasema "tuelezee"!.
" Akasema: Mtume (s.a.w.w) alipokuwa akisimama kuswali, alikuwa akiinua mikono yake mpaka iwe sawa na mabega yake, kisha anatoa Takbira mpaka kila kiungo kiwe kitulie sehemu yake huku akiwa amenyooka.
Kisha anasoma, kisha anatoa Takbira na kuinua mikono yake mpaka iwe sawa na mabega. Kisha anarukuu na kuweka viganja vyake juu ya magoti yake, kisha ananyooka bila kunyanyua kichwa chake wala kukilaza. Kisha ananyanyua kichwa chake na kusema: "(Mwenyeezi Mungu amemsikia aliyemhimidi)". Kisha ananyanyua mikono yake mpaka iwe sambamba na mabega yake mpaka kila kiungo kirudi sehemu yake huku akiwa amenyooka.Kisha anasema: "Allah Akbar".
Kisha anaporomoka (kwenda sajda) ardhini na kuweka mikono yake pembeni mwake, kisha anainua kichwa chake na kukunja mguu wake wa kushoto na kuukalia. Na anaposujudu hufungua vidole vya miguu yake. Kisha anarudi kusujudu, kisha anainua kichwa na kusema: "Allah Akbari". Kisha anakunja mguu wake na kuukalia akiwa amenyooka mpaka kila mfupa utulie sehemu yake.
Kisha anafanya hivyo katika rakaa nyingine. Kisha anaposimama toka kwenye rakaa mbili, hutoa Takbira na kuinua mikono yake mpaka iwe sawa na mabega yake kama alivyofanya pale mwanzo wa swala yake alipotoa Takbira.
Kisha anafanya hivyo hivyo katika Swala yake yote mpaka anapofika katika sijda ya kutoa salam ( ili kumaliza swala), basi hapo huchelewesha mguu wake wa kushoto na kukaa mkao wa Tawaruki na kukaa upande wake wa kushoto (yaani: Mwili ukiwa umelemea upande wa kushoto)".
Hapo wote wakasema: "Amesema kweli" ! , hakika hivyo ndivyo alivyokuwa akiswali Mtume -(s.a.w.w)- wa Mwenyeezi Mungu -(s.w)-"
((Tazama hadithi hii: Albayhaqiy: As-sunani: Juzu ya 2, ukurasa wa 72, 72,101.102. Tazama pia: At-tirmidhiy: As-sunani: Juzu ya 2, ukurasa wa 98, katika mlango wa wasifu wa Swala.Tazama pia: Musnad Ahmad: Juzu ya 5, ukurasa wa 424.))
Katika hadithi hii kuna mambo yanayoonyesha uhakika, ukweli na usahihi wa hadithi hii, moja ya mambo hayo ni Maswahaba wote hao wakubwa kumsadikisha Abu Humeidi.Kitendo hicho cha kumsadikisha kinaonyesha nguvu ya hadithi hii na usahihi wake, na kufaa kuitanguliza kabla ya kuitanguliza dalili yoyote ile nyingine. Na miongoni mwa Maswahaba wakubwa waliomsadikisha ni, Abu Hurayra, Sahl As-saidiyyu, Abu Usaydu As-saidiyu, Abu Qatadatul Haarithu bin Rabiiyu, na Muhammad bin Maslamati.
Kwa hakika Abu Humeidi As-saidiyyu, ametoa wasifu wa swala ya Mtume (s.a.w.w) kuanzia swala za Faradhi na zile za Sunna, na hajataja kufunga mikono, na wala Maswahaba hao hawajamkosoa wala kutaja kitu kingine kinyume na alivyosema, na walikuwa na nia ya kumkosoa maana pale mwanzo hawakukubali kuwa yeye ni mjuzi zaidi wa swala ya Mtume (s.a.w.w) kuliko wao.Lakini pamoja na hali hiyo,wote walisema:Umesema kweli hivyo ndivyo alivyokuwa akiswali Mtume (s.a.w.w).
Huwezi kusema kwamba makumi ya Maswahaba hao wote walisahau kumkumbusha kuwa amesahau kutaja kuwa Mtume (s.a.w.w) alikuwa "akifunga mikono"!. Dhana hii haikubaliki maana wote walikuwa katika hali na mazingira ya kukumbuka.
Ukija katika asili ya kuweka mikono, utakuta ni kuinyoosha, na hayo ndio maumbile ya Mwanadamu, na hadithi imetaja jambo linaloendana sawa na Maumbile ya Mwanadamu. Abu Humeidi As-saidiyyu hakutaja au kuonyesha isipokuwa hayo yalikuwa ni mafunzo, yaani: alikuwa katika hali ya kuonyesha au kutoa mafunzo kunako swala sahihi ya Bwana wetu Mtume (s.a.w.w), si kwamba alilenga kuwafundisha Maswahaba bali hilo lilikuwa ni somo kwa wengine na vizazi vijavyo tukiwemo sisi zama hizi.
Hivyo sifa za swala alizozitaja ndivyo hivyo swala inavyotakiwa iswaliwe na zile sifa ambazo hakuzitaja, inamaana hazitakiwi katika swala bali hiyo sio swala ya Mtume (s.a.w.w). Kwani kitendo hicho cha kutaja sifa ilikuwa ni mafunzo, hivyo huwezi kuwambia watu wenye akili zao kwamba "hakutaja jambo fulani hali ya kuwa jambo hilo ni Sunna katika swala", kwani kusema hivyo utakuwa unamaanisha Swahaba huyo (Abu Humeidi As-saidiyyu) alifanya khiyana kutotoa baadhi ya sifa, na aliyefanya khiyana si yeye tu bali hata hao Maswahaba wakubwa waliokuwa wakimsikiliza akizitaja sifa za Swala ya Mtume (s.a.w.w), nao watakuwa wamefanya khiyana maana alipomaliza kuzitaja sifa hizo na kuwaonyesha ni jinsi gani Mtume (s.a.w.w) alikiswali, walimsadikisha pasina kusema umesahau jambo la kufunga mikono!.
Kama kufunga mikono ni sunna basi ilitakiwa wamwambie, Ee bwana! Tunashukuru kwa uliyoyataja lakini Umekosea, hujataja kufunga mikono!" Na kwakuwa walimsadikisha, basi ina maana kwamba walikubaliana naye kwa zile sifa alizozitaja kuwa ndio swala sahihi aliyoiswali Mtume (s.a.w.w), na pia walikubaliana naye kwa zile sifa ambazo hakuzitaja kuwa hakika hazimo katika swala sahihi ya Bwana Mtume (s.a.w.w). Na hili la kufanya khiyana halikubaliki na liko mbali na Yeye pamoja na Maswahaba wote hao.
Hivyo ndugu Msomaji, Kwa kuwa baadhi ya Maswahaba waliokuwepo kati ya wale waliopokea hadithi za kukunja mikono, hawajapinga maelezo ya Abu Humeidi As-saidiyyu, Kwa mantiki hiyo, "kufunga mikono katika Swala" Kama ilivyo kwa Madh-hebu ya Maalik, na Alaythu bin Saad na Al-awzaiy sio Sunna katika Swala bali ni Bid'a.

Comments