HADITHI SAHIHI ZA KUNYOOSHA (AU KUACHIA) MIKONO KATIKA SWALA (KWA MUJIBU WA SHI’A

HADITHI SAHIHI ZA KUNYOOSHA (AU KUACHIA) MIKONO KATIKA SWALA (KWA MUJIBU WA SHI’A)
Hadithi ya Hammad bin Isa
Hammad bin Isa amepokea riwaya kutoka kwa Imam Jaafar Swadiq (a.s) kwamba amesema (au alisema):
Ni jambo baya sana Mtu kutimiza umri wa miaka Sitini (60) au Sabini (70) ilhali hajawahi kuswali "hata Swala moja kwa ukamilifu!"
Hammadi akasema: Ukanifikia udhalili katika nafsi yangu, nikasema: Niko chini yako, "nifundishe swala".
"Akasimama Abu Abdillah -yaani Imam Jaafar Swadiq- (a.s) huku akiwa ameelekea Qibla, akanyoosha mikono yake yote (huku akiwa ameiweka) juu ya mapaja yake ilhali kabana vidole vyake na kasogeza nyayo zake mpaka kiwango cha uwazi wa vidole vitatu, akaelekeza Qibla vidole vyake vya miguu kwa unyenyekevu pasina kuvitoa Qibla, akasema: "Allah Akbar", kisha akasoma AL-HAMDU na KULI HUWALLAH AHADU, kisha akasubiri kidogo kiwango cha kuvuta pumzi akiwa amesimama.
Kisha akasema: "Allah Akbar" akiwa amesimama, kisha akarukuu na kulaza viganja vyake kwenye magoti yaliyoachana na akarudisha magoti yake nyuma mpaka mgongo wake ukanyooka kiasi kwamba hata kama tone la maji au mafuta lingedondoka juu ya mgongo wake, basi lingekaa. Akaendelea kunyoosha mgongo huku akiwa amerudisha magoti yake nyuma, akanyoosha shingo yake mbele, kisha akamsabbihi Mwenyeezi Mungu (s.w) akisema: "Ametakasika Mola wangu Mtukufu , na kila sifa njema ni zake".
Kisha akasimama akiwa amenyooka na alipotulia akasema: "Mungu kamsikia aliyemhimidi aliyemhimidi". Kisha akatoa Takbira akiwa amesimama, akainua mikono yake mkabala na uso wake na akasujudu, akatanguliza kuweka mikono yake Ardhini kabla ya kuweka magoti yake na kusema maneno haya mara tatu: "Ametakasika Mola wangu Mtukufu na kila sifa njema ni zake".Na hakuweka sehemu ya mwili wake juu ya sehemu nyingine ya mwili wake, akasujudu.
Kisha akainua kichwa chake toka Sajda, na alipokaa sawa akasema: "Allah Akbar" akakaa kwa kulalia (kuelemea)
Upande wake wa kushoto, akawa ameweka mgongo wa mguu wake wa kulia juu ya nyayo ya mguu wake wa kushoto, kisha akasema:
((ASTAGHFIRULLAH RABIY WA ATUUBU ILAYHI))
Namuomba Mola wangu Magh-fila na ninatubu kwake".
Kisha akatoa Takbir akiwa amekaa, kisha akasujudu Sijida ya pili, akasema kama alivyosema katika Sijida ya kwanza. Wala hakutumia sehemu ya mwili wake kuusaidia mwili wake katika Sajida yake na Rukuu yake. Na wala hakuweka dhiraa zake (za mikono) juu ya Ardhi (kama afanyavyo Simba anapokuwa amelala).
Hivyo akaswali Rakaa mbili namna hii, kisha akasema:
Ewe Hammad hivi ndivyo unavyotakiwa kuswali, wala usigeuke na usicheze kwa mikono yako na miguu yako, na usiteme mate kushoto kwako au kulia kwako au mbele yako."
((Tazama riwaya hii kwenye kitabu cha Al-wasaailu cha Al-hurru Al-aamiliyyu: Juzu ya 4, mlango wa 1 ambao ni mlango wa vitendo vya swala)).
Ndugu msomaji! , kwa hakika tunapozichunguza riwaya hizi tunazikuta zinatufundisha Swala sahihi iliyoswaliwa na Bwana wetu Mtume (s.a.w.w) na amabayo Waislaam wote wanatakiwa kuiswali.
Pia riwaya hizo mbili hakuna sehemu zimetaja jambo la kufunga mikono na vigawanyo vyake tofauti.
Kama kufunga mikono ingelikuwa ni sunna, basi Imam Jaafar Swadiq (a.s) asinge sita kutenda Sunna hiyo maana kitendo chake hicho kilikuwa ni funzo kwetu sisi na kwa kila Mwislaam akitufundisha Swala sahihi ya Mbwana wetu Mtume (s.a.w.w), kwa sababu kachukua toka kwa Baba yake Imam Muhammad Baaqir (a.s), na Imam Baaqir kachukua toka kwa baba yake Imam Zainul Abidin Ali bin Hussein (a.s), na Imam Ali bin Husein (a.s) kachukua toka kwa baba yake Imam Husein (a.s), na Imam Husein (a.s) na Imam Hassan (a.s) wamechukua toka kwa Baba yao ambaye ni Imam Ali bin Abi Twalib (a.s) , na Imam Ali (a.s) kiongozi wa Waumini wote amechukua toka kwa Mtume (s.a.w.w.).
Hivyo basi "Kufunga mikono katika Swala ni Bid'a, na Bid'a maana yake ni : "Kupandikiza jambo katika sheria wakati jambo hilo halipo katika sheria !"
Tunamuomba Allah (s.w) atujalie tuwe miongoni mwa wale waliopata bahati ya kuitumia akili yao waliyopewa na Mola wao ili kutafuta Haki iko wapi na sio kuitambua tu, bali baada ya kuitambua wakaifuata.
Mtume (s.a.w.w) amesema: "Ali - (a.s) - yuko pamoja na Haki, na Haki iko pamoja na Ali -(a.s)-, (Haki) inamzunguka (Ali a.s) kwa vyovyote vile atakavyozunguka".

Comments