HAMU YA KUFA SHAHIDI

HAMU YA KUFA SHAHIDI
Amr bin Jamuh, mkazi wa Madinah na kutoka katika kabila la Khazraj, alikuwa ni mtu mkarimu na mwema.
Kwa mara ya kwanza watu wa kabila la Khazraj walipofika kwa Mtukufu Mtume (s.a.w.w), (Mtume) alitaka kujua mtu aliyekuwa kiongozi wa kabila lao. Walimjulisha kuwa alikuwa ni mtu aliyejulikana kwa jina la Jadd Ibn Qais, mtu aliyekuwa na asili ya ubahili.
Mtume (s.a.w.w) alisema: “Chifu wenu anapaswa kuwa A’mr Ibn Jamuh, mtu mweupe, mwenye nywele za mviringo.” Amr alikuwa mlemavu katika mguu wake mmoja na kwa mujibu wa sheria za Kiislamu alisamehewa kushiriki katika jihad. Alikuwa na watoto wanne wa kiume na muda wa vita vya Uhud ulipowadia, wote walijiandaa kupigana. “Lazima mimi pia nije na kupata (heshima ya) kufa shahidi, alisema Amr kwa tashwishi.” Lakini watoto wake wa kiume walimkataza na walisema, “Baba tunakwenda vitani. Kaa nyumbani kwani sio wajibu kwako kupigana.”
Baba yule mzee alikataa kubadili mawazo na akasisitiza kushiriki katika vita. Watoto wake waliwakusanya jamaa zao kwa juhudi ya kumfanya abadilishe mawazo, lakini bila mafanikio. Amr (yule baba) alimuendea Mtukufu Mtume (saw) na akamlalamikia: “Ninatamani sana kupata shahada. Kwa nini watoto wangu wananizuia kwenda kupigana jihadi na kupata shahada katika njia ya Allah?”
Mtukufu Mtume (saw) akawaambia watoto wake: “Mtu huyu anatafuta kupata shahada. Na ingawa sio wajibu kwake kupigana, haikatazwi kwake kufanya hivyo.”
Akiwa mwenye furaha kubwa, Amr alichukuwa silaha na kuelekea kwenye mapambano.
Wakati wa mapambano, watoto wake walimuangalia wakati akiwa anapambana kwa ushujaa akijitosa kwenye moyo wa safu ya maadui, akipigana kishujaa, mpaka hatimaye akauliwa shahidi.
Kabla hajaondoka kwenda uwanja wa mapambano, aliomba: “Ee Allah! Nipe mimi shahada na usinirudishe nyumbani kwangu.” Mtukufu Mtume (saw) alisema kwamba maombi yake yalijibiwa. Hatimaye Amri alizikwa kwenye makaburi ya mashahidi wa Uhud.
Rejea:
Daastaan – ha-e-Ustaad, Jz. 1. uk. 48

Comments