MALIPO YA USULUHISHI
Fudhail ibn A’yyadh amesema: Mtu mwenye sononeko la moyo alichukua kamba ambayo mke wake alikuwa ameisokota kwenda kuiuza sokoni ili kujinusuru yeye mwenyewe na familia yake kutokana na njaa.
Baada ya kuiuza kwa dirhamu moja, alikusudia kununua mkate alipokutana na watu wawili wakigombana na kurushiana makonde kwa sababu ya dirhamu moja. Mtu (yule) alisogea mbele akawapa dirhamu moja na kusuluhisha baina yao. Kwa mara nyingine tena, akiwa hana kitu mkononi, alikwenda nyumbani na kusimulia tukio zima kwa mkewe. Mkewe alifurahi kwa mwenendo wake. Alitafuta ndani ya nyumba, akapata gauni kuukuu ambalo alimkabidhi mumewe, ili aliuze na kupata chakula.
Yule mtu alilipeleka gauni sokoni lakini hapakuwa na mtu aliyekuwa tayari kulinunua. Alipotazama pembeni alimuona mtu mwenye samaki mikononi mwake. Alimwendea yule mtu na kusema, “Tubadilishane bidhaa. Nipe samaki wako nitakupa gauni langu.” Muuza samaki alikubali na yule mtu alirudi nyumbani na samaki.
Mke wake alipokuwa akijishughulisha na usafishaji wa samaki, ghafla kitu cha thamani kilitoka tumboni mwa samaki. Alimkadhi mumewe kitu hicho ili akakiuze sokoni. Mumewe alikiuza kwa bei nzuri sana na alirudi nyumbani lakini kabla hajaingia ndani mtu fukara alikuja kwenye mlango na kusema, “Nipeni kutokana na hivyo alivyokupeni Mwenyezi Mungu.” Mara tu mtu yule aliposikia wito ule, alileta fedha zote na akamtaka maskini achukue fedha anazotaka.
Muombaji alichukua fedha kiasi na akaanza kuondoka. Lakini alikuwa ametembea hatua chache tu, alirudi na kusema: “Mimi sio masikini. Nimetumwa na Mwenyezi Mungu na ninapaswa kukujulisha kuwa fedha ulizopata ni ujira wako kwa kuwasuluhisha watu wawili waliokuwa wakigombana.”
Rejea:
Namunah-e-Ma’arif, Juz. 1, uk. 218.
Namunah-e-Ma’arif, Juz. 1, uk. 218.
Comments
Post a Comment