BIBLIA NENO LA MUNGU

BIBLIA NENO LA MUNGU

Miongoni mwa nguzo za imani ya Kiislam, kuna nguzo hizi mbili, “Kuamini Manabii wa Mwenyezi Mungu na kuamini Vitabu vya Mwenyezi Mungu.” Manabii kama Musa, Daudi, Suleimani na Yesu, na wengine waliotajwa katika Biblia wote wanaaminiwa na kuheshimiwa na kila Mwislamu safi. Haiwezekani kwa muislamu kuwavunjia heshima mitume hawa au hata mmoja wao.

Waislamu wote wanaamini ya kuwa Manabii hao wote walipata ufunuo toka kwa Mwenyezi Mungu. Mara tu itakapothibitishwa ya kwamba ule ufunuo walipata wao wenyewe na kusimamia kuandikwa kwake Vitabu walipokuwa hai. Waislamu hawatasita kuukubali.

Lakini kwa bahati mbaya, maneno ya Biblia si yote yaliyofunuliwa na Mwenyezi Mungu kwa mitume wake. Historia ya Biblia inaonyesha ya kuwa hii Biblia tuliyo nayo iliandikwa kufuatia masimulizi ya nyakati mbalimbali za karne nyingi, na imefanyiwa mabadiliko makubwa, mipachiko na machafuo. Yaani mpaka zama hizi, viongozi wa makanisa hukaa na kuifanyia mabadiliko biblia bila kuona haya yoyote. Kwa vyovyote iwavyo mabadiliko haya hayawezi kuwakilisha ujumbe wa mwenyezi Mungu kwa usahihi kama ulivyokusudiwa.

Wataalamu wa Historia ya Biblia wanatuambia Agano la Kale la Kiebrania limo katika maandiko yaliyoandikwa yapata karne 5 au 8 baada ya kuondoka Yesu. Lakini hata kabla ya hapo, kwa sababu kadha wa kadha, ni wazi kwamba michafuo mingi ilifanywa ndani ya maandiko hayo ya Kiebrania (Encyclopaedia Britanica, Chapa ya II - chini ya neno Bible). Hili ndiyo hali ya Agano la Kale.

Hebu sasa tulichunguze Agano Jipya lililoandikwa baadaye na ndiyo maandiko matakatifu ya Wakristo.

Mtaalamu mashuhuri wa huko Oxford ameandika haya katika kitabu chake “The Story Behind the Gospel” yaani (Hadithi ya Undani wa Injili). “Jambo la maana ni kukumbuka ya kuwa hakuna hata Injili moja iliyopata kuandikwa mpaka miaka mingi sana baada ya kujificha cha Yesu. Kwa ujumla Injili ya Marko ndiyo inayodhaniwa kuwa ya zamani zaidi. Inakadirwa kuwa iliandikwa mnano 65 A.D. baada ya kuzaliwa Yesu. Tarehe ya kusulubiwa kwa Yesu inafikiriwa kuwa mwaka 29 au 30 A.D. Hivyo Injili hii iko kama miaka 35 hivi nyuma ya habari inazozieleza. Injili zilizobaki ziliandikwa miaka mingi baadaye.

“Katika miaka ya mwanzo iliyofuatia kifo cha Yesu hapakuwepo na maandiko yoyote juu ya maisha na mafundisho ya Yesu. Pengine baadhi ya methali zake mashuhuri zilikuwa zimeingizwa katika ibara fulani fulani. Lakini kadri miaka ilivyozidi kupita na maneno ya Yesu kuzidi kusahaulika ilionelewa heri kuyaandika.

Usahihi wa maandiko hayo awali ulikuwa ni lazima utegemee maoni ya wale walioweza kukumbuka maneno ya Yesu, kama ilivyokuwa zama zile, na pia masimulizi ya wale waliokua na Yesu na kumsikia, na Injili za leo zimeandikwa kufuatia visa na masimulizi haya.

Ukweli ni kuwa habari, hata ikiwa ni juu ya jambo lililotendeka hivi punde tu, ni vigumu sana kupita kinywa hata kinywa bila ya kupata mabadiliko. Hivyo linakuwa ni jambo lisilopingika ya kwamba masimulizi ya Yesu yalivyopitia kinywa hiki hadi kile kwa muda wa miaka thelathini (katika zama za giza) yalipata mabadiliko makubwa katika muda huo wote.

Kadhalika yatupasa tukumbuke ile desturi ya waandishi wa kale, kwani wao walipoandika habari za mtu fulani walitumia maneno waliyoona yanatimiza mradi wao bila ya kukusudia kudokeza ya kuwa hayo ni sahihi na ni yale yale aliyoyatamka yule mtu mwenyewe. Wala hapakuwa na mwandishi wa kale aliyekuwa mwangalifu hivi kwamba aliyachungua na kuyakariri maandiko yake hata yakaweza kufafanua mradi kamili wa jambo alilokusudia kueleza.

Bila shaka Injili, ambazo hazikuandikwa kama kumbukumbu tu bali kama mafundisho pia, zilihusikana sana na tabia hii ya mwandishi wa kale. Kwa hivyo hatuna usalama wowote ya kuwa visa na methali kama tusomavyo katika Biblia zinawakilisha matendo hasa yaliyotendeka na maneno ya asili yaliyonenwa,” (The Story Behind the Bible, by Mr. Allen, ukurasa 44).

Kwa maana hii, Biblia ni hati iliyoandikwa na watu kufuatia mila na methali iliyorithiwa toka kizazi hata kizazi. Karne nyingi zilipita kabla Biblia haijaingia katika sura yake ya hivi sasa, na katika muda huo mrefu, ilifanyiwa mabadiliko mengi, mipachiko na machafuo chungu nzima. Katika hali hii Biblia kimekuwa kitabu kinachokusanya ukweli uliochanganyika na uzushi, upungufu na maneno yasiyopatana.

Baadhi ya ukweli uliomo Bibliani, ni bishara ambazo katika hizo nyingi zilitimia kwa kufika kwake Mtume Muhammad (s.a.w.w), kunako majaliwa ya Allah, nitazieleza taratibu tena kwa umakini mkubwa.

Kuja kwa Nabii Muhammad (s.a.w.w) si jambo geni kwa watu wa kitabu maana kumebashiriwa mara nyingi katika Biblia. Haya yanathibitishwa na Qur’an Tukufu inayosema hivi juu ya waaminio kwamba ni wale “Ambao wanamfuata Mtume, Nabii aliye Ummi, ambaye wao humkuta ameandikwa kwao katika Taurati na Injili. Huwaamuru yaliyo mema na kuwakataza yaliyo mabaya.” (7:158).

Maneno haya “Ameandikwa kwao katika Taurati na Injili”, yanaonyesha kwamba Nabii Muhammad (s.a.w.w) si Mtume wa kitaifa bali ametumwa kwa mataifa yote ya wanadamu. Yeye ni mbora wa mitume wote (Sura 33:41) naye alitumwa kwa watu wote (Sura 7:159) bishara zinazotabiri kuja kwake zinapatikana katika vitabu vya dini zote. Hapa vimetajwa Taurati na Injili. Katika vitabu hivyo mna bishara nyingi zenye kuwawezesha Mayahudi na Wakristo kumtambua Mtume Muhammad (s.a.w.w).

Hii ni tofauti kabisa na Qur’an ambayo iliandikwa kwa usimamizi wa Mtume mwenyewe katika uhai wake. Alifariki mtume anakiacha kitabu kikiwa kimekamilika, ikawa ni jukumu la waislamu kukihifadhi tu.

Comments