HADITH YA KARATASI

HADITH YA KARATASI

Hii ni Hadith iliyo mashuhuri sana. Wanazuoni wa Hadith  wameitaja katika vitabu vyao, na vile vile wanahistoria kadha wa kadha wameitaja katika vitabu vyao. Na kati ya wote hao hakuna hata mmoja aliyekikanusha kisa hicho, wala kukitilia shaka.
Kati ya vitabu vya Hadith vilivyosimulia kisa hiki ni Sahih Bukhari. Kwa masunni, hiki ndicho kitabu kilicho sahihi mno, na kwa hivyo kuaminiwa mno, baada ya Qur’ani Tukufu. Katika kitabu hicho mna riwaya saba zinazosimulia kisa hicho. Kwa faida ya  wasomaji wetu, hapa chini tunazidondoa zote:

1.    Imepokewa kwa Ibn Abbas akisema: “Mtume (s.a.w.w.)  alipozidiwa na maradhi yake, alisema: Nileteeni (karatasi  ya) kuandikia, niwaandikie maneno ambayo baada yake  hamutapotea. Lakini Umar akasema: Hakika Mtume (s.a.w.w.) amezidiwa na maradhi, na sisi tunacho Kitabu cha Mwenyezi Mungu. Kinatutosha. Hapo basi (maswahaba) wakakhitalifiana,  na zogo likazidi, (Mtume s.a.w.w.) akasema: Niondokeeni!  Haifai kuzozana mbele yangu.”

Ibn Abbas akatoka huku anasema: “Msiba ulioje wa Mtume (s.a.w.w.) kuzuiwa kuandika (alichotaka kuandika).”
Hadith hii imo katika Kitaabul Ilm, Mlango wa Kitaabatil Ilm. Kwa tafsiri ya Kiingereza ya kitabu hicho, ni Hadith Na. 114, uk. 86 wa Juzuu ya Kwanza.

2.    Imepokewa kwa Said bin Jubayr kwamba alimsikia Ibn Abbas r.a. akisema: “Siku ya Alkhamisi! Na ni ipi hiyo siku ya  Alkhamisi?” Kisha akalia mpaka mawe yakaroa kwa machozi  yake.

Nikamuuliza: “Ewe Ibn Abbas! Ina nini hiyo siku ya Alkhamisi?” Akasema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) alizidiwa na maradhi yake. Akasema: Nileteeni mfupa wa bega niwaandikieni maneno ambayo baada yake hamutapotea  abadan. (Maswahaba) hapo wakazozana, wala haifai  kuzozana mbele ya Mtume s.a.w.w. Na wakauliza: Ana nini?  Anaweweseka? Muulizeni (ili mujue hali yake). Yeye s.a.w.w.  akasema: Niacheni! Niliyonayo ni bora kuliko hayo  munayonitaka nyinyi niyafanye.

“Hapo (Mtume s.a.w.w.) akawaamrisha mambo matatu. Akasema: Watoeni Bara Arabu washirikina wote, wapeni zawadi wajumbe (wa kigeni wanapokuja kwenu) kama nilivyokuwa nikiwapa mimi. Msimuliaji akaongeza: “La tatu ni jambo la kheri ambalo ama Ibn Abbas alilinyamaza, au alilitaja lakini nimelisahau!”
Hadith hii imo katika Kitaabu Fardhil Khumsi, Mlango wa Ikhraajil Yahudi Min Jaziratil Arab. Kwa Kiingereza ni Hadith No. 393, uk. 260 wa Juzuu ya Nne.


3.    Maneno ya hii Hadith ya tatu karibu yote ni sawa na yale ya Hadith Na. 2 hapo juu. Nayo imo katika Kitaabul Maghaazil, Mlango wa Maradhin Nabiyyi (s.a.w.w.) wa Wafaatihii. Kwa Kiingereza, ni Hadith Na. 716, uk. 511 wa Juzuu yo Tano.

4. Imepokewa kwa Ubaydullah kwamba Ibn Abbas r.a.  amesema: “Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) alipouguwa maradhi ambayo ndiyo aliyofia, na nyumbani mwake mkawa muna watu akiwamo Umar miongoni mwao, alisema: Njooni niwaandikie maneno ambayo hamutapotea baada yake. Umar akasema: Hakika Mtume s.a.w.w. amezidiwa na maradhi, na  nyinyi munayo Qur’ani. Kinatutosha Kitabu cha Mwenyezi  Mungu. Watu waliokuwapo hapo nyumbani wakazozana. 

Wengine walisema: Njooni karibu ili Mtume (s.a.w.w.)  atuandikie maneno ambayo hatutapotea baada yake. Na wengine wakasema alivyosema Umar. Walipozidisha zogo lao na ikhtilafu zao mbele ya Mtume (s.a.w.w.), Mtume wa  Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) alisema: Niondokeeni!
“Ubaydullah anasema: Ibn Abbas alikuwa akisema: Msiba ulioje  wa Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w.) kuzuiwa kuyaandika  maneno haya kwa sababu ya ikhtilafu zao na zogo lao.”

Hadith hii imo katika Kitaabul Mardhwaa, Mlango wa Qawlil  Mariidhwi Quumuu Annii. Kwa Kiingereza ni Hadith Na. 573,  ukurasa wa 389 wa Juzuu ya Saba.

4.    Maneno ya hii Hadith ya tano karibu yote ni sawa na yale ya Hadith Na. 4 hapo juu.

Nayo imo katika Kitaabul I’tiswaami Bil Kitaabi was Sunnah, Mlango wa Karaahiyatil Ikhtilaaf. Kwa Kiingereza ni Hadith Na. 468, ukurasa wa 346 - 347 wa Juzuu ya Tisa.

Kitabu kingine kinachosimulia Hadith hii ni Sahih Muslim.  Kitabu hiki, kwa masunni, ndicho cha pili (baada ya Sahih Bukhari) kilicho sahihi mno baada ya Qur’ani Tukufu. Maneno ya Hadith  iliyomo humu ni karibu sawa na yale yaliyonukuliwa na Bukhari katika Hadith Na. 2 hapo juu.


Hapa ningependa tukumbushane wanavyosema wanazuoni wa  kisunni wa fani ya Hadith. Wao wanasema: Iwapo Hadith imepokewa na Bukhari na Muslim (wote wawili pamoja), basi  Hadith hiyo huhisabiwa kuwa i sahihi mno (mu’tafaq alayhi). Ya pili kwa usahihi ni ile iliyopokewa na Bukhari peke yake. Ya tatu ni ile ya Muslim pekee.  

Comments