UTABIRI WA PILI WA MTUME MUHAMMAD NDANI YA BIBLIA

UTABIRI WA PILI WA MTUME MUHAMMAD NDANI YA BIBLIA

Katika kumbukumbu la Taurati 33:2-3 imeandikwa hivi, “Bwana
alitoka Sinai, akawaondokea kutoka Seiri, akaangaza kutoka kilima
cha Parani, na akaja na elfu kumi za watakatifu. Upande wa mkono
wake wa kuume palikuwa na sheria ya moto moto kwao. Hakika
awapenda hayo makabila ya watu, watakatifu wake wote wamo
mkononi mwako, nao waliketi miguuni pako”.

Hapa pameelezwa maonyesho matatu ya Mwenyezi Mungu.
1.     Musa alitoka Sinai.
2.     Seiri ni alama ya Yesu.
3.     Na Mtume Muhammad s.a.w. aliangaza kutoka kilima cha Parani.

Wanazuoni wamekubali ya kwamba Parani ni kilima cha Makka (Mu’jamul Buldaan).

Biblia inasema. Ismaili “akakaa katika jangwa la Parani” (Mwanzo 21:21)
na Mtume Muhammad (s.a.w.w) ni mjukuu wa lsmaili. Huu ni ushahidi kuwa aliyekusudiwa hapa ni Mtume Muhammad (s.a.w.w).
Mtume s.a.w. alipoondoka Madina kwenda kuiteka Makka alikuwa na masahaba elfu kumi. Katika Biblia ya Kiingereza hesabu ya watakatifu hao imetajwa kuwa “ten thousand saints” yaani “watakatifu elfu kumi”, kama tulivyofasiri hapo juu.

Lakini katika Biblia ya Kiswahili cha Mvita (Mombasa). Wamefasiri maneno hayo kuwa “Makumi ya elfu”, yaani elfu zile zilikuwa si kumi moja bali
makumi mengi, wapate kuwavuruga wasomao Kiswahili wasijue hesabu ya Masahaba watakatifu wa (Mtume s.a.w.w) aliotokea nao Parani katika utabiri wa Biblia. lnasikitisha kuona ya kwamba Mapadri na wachungaji hawajatosheka na kiasi hicho cha uchakachuzi. Katika tafsiri mpya ya Biblia (Union Version) ya mwaka 1952 kifungu hicho cha maneno wamekiandika: “Akaja Meribath kadeshi”, ili wavuruge kabisa utabiri huyo usiweze kufafanuka. Ni ajabu maneno kama Tirshatha (uk. 478), Darkoni (uk. 479) na mengine yametafsiwa chini katika kurasa, na mengine yametafsiriwa mwisho wa kitabu cha Biblia, lakini neno Meribath-kadeshi hawakulieleza chini ya ukurasa ule wala mwisho wa kitabu. Ingawa ni jipya kabisa lakini
limefanywa lionekane kama jina la mtu au Malaika au vinginevyo.

Wale wanaofikiri ya kwamba Biblia ya Union Version imefasiriwa vizuri
sana katika Kiswahili cha kisasa, watasemaje juu ya uaminifu huu wa wafasiri? llikuwaje wanazuoni wakubwa wakubwa wa Kiyunani na Kiebrania na Kiswahili kushindwa kufasiri au kueleza neno Meribath -kadeshi? Inaonekana dhahiri ya kwamba dhamiri za mapadri zinawalaumu juu ya tafsiri zao zisizo sahihi, zinazovurugwa ili kuficha haki.

Alama nyingine ni kuleta Sheria. Mtume Muhammad s.a.w. ndiye aliyeleta Sheria baada ya Nabii Musa. Na ile Sheria ilileta joto katika mioyo ya Waislamu, nao wakainuka katika miaka michache. Pia imeitwa “Sheria ya Moto Moto” kwa ajili ya kuunguza maovu, madhambi na mabaya yote. Wale waliojaribu kuipinga Kurani wakaangamia wenyewe. Kweli, Kurani ikifuatwa sawa sawa, inaweza kuchoma dhambi za watu kama moto unavyochoma takataka. Je hamwoni Waarabu waliokuwa wakinywa ulevi kutwa mara tano waliacha wakawa wanasali kutwa mara tano?

Mtume alizipenda sana kabila zote. Katika masahaba wake kulikuwa Watu wa makabila mbali mbali: Waarabu, Wahabeshi, Waajemi na Warumi, na Mtume (s.a.w.w) aliwapenda wote. Hakuwaita mbwa na nguruwe watu wa mataifa mengine kama alivyowaita Yesu (Mathayo 7:6; 15:26).

Masahaba wa Mtume (s.a.w.w) pia walimpenda sana. Kwa hakika Mtume (s.a.w.w) alipendwa na masahaba zake zaidi kuliko kila mtu anavyopendwa na wafuasi wake. Katika vita, kama mishale ilipigwa kutoka katika kila upande, masahaba walimzunguka Mtume kama kuta ili asipate kujeruhiwa. Hatuwezi kuwalinganisha na wanafunzi wa Yesu waliomtoroka wote wakakimbia na kumwacha Yesu peke yake katika matata (Mathayo 26:56. Marko 14:50).


Ninawakaribisha watu wote katika Uislamu kwa sababu ndio dini sahihi iliyotabiriwa katika vitabu vilivyotangulia. Kunako majaliwa ya Allah nitaleta tabiri nyingi zingine kutoka katika vitabu vya kikrito, kiyahudi, kibudha na hata kihindu. 

Comments