MAELEZO YA MASHIA KUHUSU
MWANZO WA WAHYI
Assalaam alaykum:
Waislamu wa Shia, wanaamini
kuwa mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w), alipofikia na malaika Jibril siku
aliyomtokea kwa mara ya kwanza, alimkaribisha kama aliyekuwa akimtarajia.
Jibril alimletea zile habari njema kwamba Allah (s.w.t.) amemchagua yeye kuwa
Mtume Wake wa mwisho kwa wanadamu na akampongeza kwa kuteuliwa kuwa mpokeaji wa
heshima kubwa kuliko zote kwa mwanadamu katika dunia hii.
Mtume Muhammad (s.a.w.w)
hakusita katika kuupokea ujumbe wa Utume wala hakuwa na ugumu wowote katika
kurudia zile Aya za Wahyi wa mwanzo. Alizisoma au kuzirudia bila ya taabu
yoyote, mwenyewe. Jibril, kwa kweli, hakuwa mgeni kwake, na alijua pia kwamba
sababu ya kuwepo kwake mwenyewe ilikuwa ni kutekeleza ujumbe uliowekwa juu yake
na Allah (s.w.t.) kama Mtume Wake. Alikuwa “mwenye kuuelewa ujumbe” hata kabla
ya kufika kwa Jibril.
Waislamu wa Shia pia
wanasema kwamba kitu kimoja ambacho Jibril hakuwa akifanye, kilikuwa ni kutumia
nguvu za kimwili juu ya Mtume kusoma. Kama alifanya, itakuwa kwa kweli ni
mtindo wa ajabu wa kumpa mtume Muhammad (s.a.w.w) huo uwezo wa kusoma – kwa
kumminya au kumkaba. Wanasisitiza zaidi kwamba Mtume hakuazimia kujiuwa katika
wakati wowote wa maisha yake, sio hata katika nyakati za huzuni sana; na kwamba
haijawahi kumjia kwamba angeweza kamwe kuguswa na “uovu” au kwamba angeweza
“kupotoshwa” au “kuchafuliwa.”
Hata hivyo, Mtume alihisi
wasiwasi juu ya ukubwa wa jukumu lililo mbele yake. Alitambua kwamba katika
utekelezaji wa kazi yake, atakuja kukabiliwa na upinzani mkubwa, mgumu, na
uliodhamiriwa wa mapagani wa dunia nzima. Ile hali ya wasiwasi wake ilikuwa
karibu kudhihirika.
Alikuwa, kwa hiyo, kwenye
hali ya uzito wa mawazo alipoondoka pale pangoni kurudi nyumbani. Na alimuomba
Khadija kumfunika ndani ya blanketi wakati akikaa chini kumuelezea yale matukio
ya kule Hira.
Khadija alipoisikia Hadith
aliyomwambia Mtume, alimliwaza na kumpa moyo kwa kusema, “Ewe mwana wa ami
yangu, kuwa mwenye furaha nzuri, Allah (s.w.t.) amekuchagua wewe kuwa Mtume
Wake. Wewe siku zote ni mpole kwa majirani zako, mwenye msaada kwa jamaa zako,
mkarimu kwa mayatima, wajane na masikini, na mwenye upendo kwa wageni. Allah
(s.w.t.) kamwe hatakuacha wewe peke yako.”
Inawezekana kwamba Muhammad
alizidiwa kwa muda kidogo na mawazo juu ya uwajibikaji wake kwa Allah (s.w.t.)
katika kuubeba mzigo mzito wa jukumu lake jipya, lakini pale aliposikia maneno
ya kuliwaza ya Khadija (mama wa waumini), mara moja alijisikia zile fadhaa zote
ndani yake zikipungua. Alimtuliza na kumpa moyo kwamba pamoja na Mkono wa Allah
(s.w.t.) juu ya bega lake, atasimama sawia na majukumu yake na ataweza kushinda
vikwazo vyote.
Comments
Post a Comment