UPOTOFU YA UWAHHABI KUHUSU MWANZO WA WAHYI

Assalaam alaykum:

Maelezo ya Hadith ya Kisalafi juu ya tukio hili nimeyanukuu kutoka katika makala iliyoandikwa na Sheikh Ahmad Zaki Hammad, Ph.D, yenye kichwa cha habari Be hopeful, iliyochapishwa kwenye jarida la kila mwezi, Islamic Horizons la Jamii ya Kiislam ya Amerika Kaskazini, Plainfield, Indiana, la Mei-Juni 1987, kama ifuatavyo:

“Mtume (s.a.w.) katika hatua za mwanzo huko Makka, alipotokewa na malaika Jibril, alihofia kwamba ile hali ya Wahyi ilikuwa ni mguso wa uovu uliokuwa ukimuwinda, ukimchezea kiakili, kutibua utulivu wake na amani ya mawazo. Alihofia kwamba huenda moja ya majini limemgusa. Alilieleza hili kwa Khadija. Hofu yake ilizidi kufikia kiasi kwamba - na tafadhali usishangazwe na Hadith sahihi ndani ya Bukhari – Mtume (s.a.w.) alitamani kuua nafsi yake kuliko kuguswa na uovu, kuchezewa, kupotoshwa, au kuchafuliwa.”

Amma alipoambia asome Qur’an (96:1-5) alishindwa kusoma kiasi kwamba ilibidi malaika Jibril ambane sana na kumlazimisha kufanya hivyo, hali ambayo ilimwongezea hofu, maumivu na mashaka.

Lakini kulingana na maelezo ya Waislamu wa Shia, mtume Muhammad Mustafa, kinyume na kushutushwa au kuhofishwa na kutokea kwa Jibril, alimkaribisha kama aliyekuwa akimtarajia. Jibril alimletea zile habari njema kwamba Allah (s.w.t.) amemchagua yeye kuwa Mtume Wake wa mwisho kwa wanadamu na akampongeza kwa kuteuliwa kuwa mpokeaji wa heshima kubwa kuliko zote kwa mwanadamu katika dunia hii.


Mtume Muhammad (s.a.w.w) hakusita katika kuupokea ujumbe wa Utume wala hakuwa na ugumu wowote katika kurudia zile Aya za Wahyi wa mwanzo. Alizisoma au kuzirudia bila ya taabu yoyote, mwenyewe. Jibril, kwa kweli, hakuwa mgeni kwake, na alijua pia kwamba sababu ya kuwepo kwake mwenyewe ilikuwa ni kutekeleza ujumbe uliowekwa juu yake na Allah (s.w.t.) kama Mtume Wake. Alikuwa “mwenye kuuelewa ujumbe” hata kabla ya kufika kwa Jibril.

Comments