WAHYI WA PILI KUSHUKA KWA MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W)

WAHYI WA PILI KUSHUKA KWA MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W)

Assalaam alaykum:

Tokea Mtume alipokea wahyi wa kwanza kwa furaha, kilipita kipindi kifupi tu, Jibril akatokea tena mbele ya mtume Muhammad (s.a.w.w) wakati alipokuwa ndani ya pango la Hira, na akawasilisha kwake wahyi wa pili:

“Ewe uliyejifunika (shuka). Simama na uonye. Na Mola wako mtukuze. (Sura ya 74; Aya ya 1-3).

Hii amri kutoka Mbinguni ya “simama na uonye” ilikuwa ni ishara kwa mtume kuanza kazi yake.

Jibril alimweleza yeye kazi zake mpya ya kwanza kabisa ilikuwa ni kuangamiza ibada ya miungu ya uongo, na kusimamisha beramu ya Tawhid - imani ya Upweke wa Muumba – ulimwenguni; na alikuwa awaite wanadamu kwenye dini ya Haki – yaani Uislamu.

Uislamu maana yake ni kunyenyekea kwa Allah (s.w.t.) na kumkubali Muhammad kama mja na Mtume Wake.

Jioni ile mtume alirudi nyumbani mwenye fahamu na dhamira juu ya kazi yake mpya kwamba alikuwa anapaswa kuutangaza Uislamu, na kwamba alikuwa aanzie kutoka nyumbani kwake mwenyewe  kwa kuutangaza kwa mkewe.

Mtume alimweleza bi Khadija juu ya kutembelewa kwa mara ya pili na Jibril, na wajibu uliowekwa juu yake na Allah (s.w.t.) wa kumwita yeye Khadija kwenye Uislamu. Kwa Khadija, historia na ukamilifu wa uadilifu wa mume wake vilikuwa ni uthibitisho usiopingika kwamba alikuwa ni mjumbe wa ki-ungu, na aliukubali Uislamu bila kusita. Kwa kweli, kati yake na Uislamu, kulikuwa na “uhusiano wa kiitikadi” fulani uliokuwepo kabla.

Kwa hiyo, wakati Muhammad Mustafa (s.a.w.w) alipoleta Uislamu kwake, Khadija “aliutambua” mara moja, na akaufuata kwa matumaini. Aliamini kwamba Muumba ni Mmoja, na kwamba Muhammad alikuwa ni Mtume Wake, naye akatamka:
“Nashuhudia kwamba hakuna mungu ila Allah (s.w.t.); na ninashuhudia kwamba Muhammad ni mtumwa na Mtume Wake.”

Muhammad; huyu Mtume mpya wa Mungu, alijishindia mfuasi wake wa kwanza - Khadija– mke wake. Alikuwa ndiye wa kwanza, wa kwanza kabisa kuthibitisha imani yake katika Tawhid (Upweke wa Muumba), na alikuwa ndiye wa kwanza kabisa kumkubali Muhammad kama Mtume wa Allah (s.w.t.) kwa wanadamu wote. Alikuwa ndio Mwislamu mwanamke wa kwanza.

Imam Ali Ibn Abi Talib, alikuwa akiishi wakati huu na walezi wake, mtume Muhammad na Khadija. Wale vijana wawili wa Muhammad na Khadija – Qasim na Abdullah walikwisha kufa katika uchanga wao. Baada ya kifo chao, walimchukua Ali kama mtoto wao. Ali alikuwa na umri wa miaka mitano alipokuja nyumbani kwao, na alikuwa na miaka kumi pale mtume Muhammad (s.a.w.w) alipotangazwa Mtume wa Allah (s.w.t.) Muhammad na Khadija walimlea na kumsomesha.

Kwa kuwa imam Ali alikuwa mmoja wa familia ya Mtume (s.a.w.) mwenyewe, alikuwa bila ya kukwepa, wa kwanza miongoni mwa wanaume kuupokea ujumbe wa Uislamu. Alishuhudia kwamba Mungu ni Mmoja, na kwamba Muhammad alikuwa Mtume Wake. Na alikuwa na shauku ya kusimama nyuma ya mtume kuswali. Kwa vile mtume hakuonekana kamwe kwenye Swala isipokuwa pale imam Ali alipokuwa pamoja naye.


Mvulana huyu pia alihifadhi Aya za Qur’an Tukufu kila pale ziliposhushwa kwa mtume. Kwa namna hii, alikua hasa na Qur’an. Kwa kweli, Ali na Qur’an “vilikuwa” pamoja kama “mapacha” ndani ya nyumba ya mtume Muhammad Mustafa (s.a.w.w) na Khadija-tul-Kubra (a.s). Mtume wa Allah (s.w.t.) alikwishapata mwislamu wa kike wa kwanza kwa Khadija, na mwislamu wa kwanza wa kiume kwa Ali Ibn Abi Talib (a.s).

Comments