HISTORIA YATHIBITISHA IMAM ALLY MWISLAMU WA KWANZA.

Mwanahistoria Muhammad Ibn Is’haq Anatuambia:
“Ali alikuwa ndiye mwislamu wa kwanza kumwamini Mtume wa Allah (s.w.t.) kuswali naye na kuuamini ujumbe wake mtukufu, alipokuwa ni mvulana wa miaka kumi. Mungu alimpendelea kwa vile alilelewa katika uangalizi wa Mtume (s.a.w.) kabla Uislamu kuanza rasmi.”(The life of the Messenger of God).

Mwanahistoria mwingine Muhammad Husein Haykal Naye Asema:
“Hivyo basi Ali alikuwa ndio kijana wa kwanza kuingia Uislamu. Alifuatiwa na Zayd ibn Harithah, mtumishi wake Muhammad. Uislamu ulibakia umefungiwa ndani ya kuta nne za nyumba moja. mbali na Muhammad mwenyewe, wafuasi wa dini mpya walikuwa ni mkewe, binamu yake, na mtumishi wake.” (The Life of Muhammad, Cairo, 1935).

Marmaduke Pickhtalls, anasema:
“Wa mwanzo kati ya wafuasi wake (Muhammad) alikuwa ni mke wake, Khadija; wa pili binamu yake wa kwanza Ali, ambaye alimtwaa (kumlea); wa tatu mtumishi wake Zaid, aliyekuwa mtumwa hapo awali.”(Introduction to the Translation of Holy Qur’an, Lahore, Pakistan, 1975).
Kisha anaendelea, Shahidi wa tatu kuukubali Uislamu, alikuwa Zayd ibn Harithah, huria wa Muhammad, na mtu wa nyumba yake.

Tor Andre anatwambia kuwa: “Zayd alikuwa mmoja wa watu wa mwanzo kuukubali Uislamu, kwa kweli alikuwa wa tatu, baada ya Khadija na Ali.” (Muhammad, the Man and his Faith, 1960).

Ibn Ishaq anatuhadithia kuwa: “Kutoka kwa Yahya ibn al-Ash’ath ibn Qays al-Kindi kutoka kwa baba yake, kutoka kwa babu yake Afiif: anasema Al-Abbas ibn Abdul Muttalib alikuwa rafiki yangu aliyekuwa akienda mara kwa mara Yemen kununua manukato na kuyauza wakati wa maonyesho.
Nilikuwa pamoja naye huko Mina, alikuja mtu katika ujana wa maisha yake na akatekeleza kanuni zote za wudhu’u na kisha akasimama na kuswali. Kisha akatoka mwanamke akachukua wudhu’u na akasimama na kuswali. Kisha akatoka kijana anayekaribia utu uzima, akachukua wudhu’u, kisha akasimama na akasali kando yake.

Nilipomuuliza Al-Abbas ni nini kilikuwa kinaendelea, akasema kwamba alikuwa ni mpwa wake Muhammad Ibn Abdullah Ibn Abdul Muttalib, anayedai kwamba Allah (s.w.t.) amemtuma kama Mtume; yule mwingine ni mtoto wa ndugu yangu, Ali Ibn Abi Talib, ambaye amemfuata katika dini yake; yule wa tatu ni mke wake, Khadija binti ya Khuwaylid ambaye pia anamfuata katika dini yake. Afiif alisema baada ya kuwa amekuwa mwislamu na Uislamu ukiwa umejengeka imara moyoni mwake‘Laiti mimi ningekuwa wa nne!’ (The Life of the Messenger of God).

Shahidi wa nne aliyeukubali Uislamu, ni Abu Bakr, mfanya biashara wa Makka.

Hapo mwanzoni, Muhammad alihubiri Uislamu kwa siri kwa hofu ya kuamsha uhasama wa waabudu masanamu. Aliwaita tu wale watu kwenye Uislamu ambao alijuana nao yeye binafsi. Inasemekana kwamba kwa juhudi za Abu Bakr, huyu mwislamu wa nne, watu wengine wachache wa Makka pia waliukubali Uislamu. Miongoni mwao walikuwa Uthman bin Affan, Khalifa wa baadae wa Waislamu; Talha, Zubayr, Abdur Rahman bin Auf, Saad bin Abi Waqqas, na Ubaidullah ibn al-Jarrah.
Kwa muda mrefu Waislamu walikuwa wachache kwa idadi na hawakuthubutu kuendesha Swala zao hadharani. Mmoja wa wafuasi wa mwanzo wa Uislamu alikuwa ni Arqam bin Abi al-Arqam, kijana wa ukoo wa Makhzuum.

Alikuwa tajiri na akiishi katika nyumba yenye nafasi kubwa katika bonde la Safa. Waislamu walikusanyika kwenye nyumba yake kuswali Swala zao za jamaa. Miaka mitatu ikapita kwa namna hii.

Comments