UTABIRI WA TANO WA MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W) NDANI YA BIBLIA.

UTABIRI WA TANO WA MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W) NDANI YA BIBLIA.

Katika Isaya (21.13-17) mmeandikwa: “Hili ni neno zito lililo juu ya Arabia. Ninyi mtalala ndani ya msitu wa Arabuni, enyi Wadedani wenye kusafiri pamoja, Wenyeji wa nchi ya Tema walimletea maji yule aliyekuwa na kiu, walimlisha mkate wao yule aliyekimbia.
“Kwani walizikimbia hizo panga, huo upanga uliofutwa, na huo uta uliopindwa, na hayo mazito ya vita. Kwani yeye Jehova ameniambia neno hili, katika muda wa mwaka mmoja, kwa kuandama hesabu ya miaka ya mwenye kuajiriwa, huo utukufu wote wa Kedari utabatilika, na hao watakaosalia katika hesabu ya hao wenye kutumia uta, hao Mashujaa wa hao wana wa Kedari, watakuwa ni wachache kwa maana Jehova, yeye Mwenyezi Mungu wa Israeli, amenena neno hili.”

1.     Aya 13 inatabiri juu ya “Hijra” yaani kuhama kwa Mtume Muhammad (s.a.w.) kutoka Makka hadi Madina. Tukio hili ni mojawapo katika matukio matukufu sana katika historia ya dini ya Kiislamu, maana Kalenda ya Kiislamu huanzia tangu wakati huo. Mtume s.a.w. alipotoka Makka kwa amri ya Mwenyezi Mungu na kuhamia Madina ambako alistawi sana na baadaye akiwa na masahaba wake watakatifu elfu kumi alirudi kuingia Makka bila kizuizi.

2.     Maneno ya Aya 14 yanaeleza hali ya Mtume (s.a.w.) aliposafiri kuhamia Madina. Ikumbukwe ya kwamba Tema ndilo jina la nchi ambamo miji ya Makka na Madina yapatikana.

3.     Maelezo ya aya 15, ni juu ya ile hali ya nchi yenye mateso na usumbufu juu ya Mtume (s.a.w.) ambayo watu wa Makka walimtendea hata maisha yake yakawa katika hatari katika mji huo alimozaliwa. Katika kitabu cha Maisha ya Mtume Muhammad, kilichoandikwa na marehemu Al-Haj F. R. Hakeem uk. 22 imesimuliwa hivi :-

“Mwisho saa ilifika. Wakimkuta Mtume (s.a.w.) akielekea kuwa peke yake kabisa, Wakubwa wa Kikureshi walifanya mkutano katika Dar-un-Nadwa.. ambako mambo ya kiserikali yalifikiriwa na mashauri kukatwa. Walikutana huko na kushauriana jambo gani afanyiwe. Baadhi yao walifikiri afungwe kamba na atupwe katika chumba cha giza na aachwe bila chakula mpaka afe.

Wengine walifikiri asafirishwe mbali sana. Lakini, mwishowe Abu Jahli aliwapa mawazo yake ya kwamba vijana wa ukoo mkuu wapewe panga kali, ambao watatumia kwa kumhujumu kwamba wote watamshambulia wakati mmoja ili pasiwe na kabila maalumu la Makureshi la kushtakiwa kwa kuua. Bani Hashim (Kabila la Mtume, s.a.w.) lingeridhika, kwa hivyo kupewa pesa za damu badala ya kuwaadhibu.

“Mpango huu ulikubaliwa na watu wote. Baadaye watu walio na silaha walijipanga nje ya nyumba ya Mtume (s.a.w.) tayari kumuua akitoka nje. Lakini Mwenyezi Mungu alimwepusha na hila zao mbaya na akamwepusha na panga zao zilizokuwa kali.”
Hii ndiyo iliyokuwa hali ya mji wa Makka Mtume alipouhama, na hizi hasa ndizo hali zilizotabiriwa na maneno hayo ya Isaya.

4.     Aya 16 yatabiri juu ya vita vya Badr, ambavyo Mtume (s.a.w.) na wafuasi wake wachache walipigana na kundi kubwa la maadui wa Uislamu mwaka mmoja baada ya Mtume kuhamia Madina.

Katika vita hivi vilivyopiganwa karibu na mji wa Madina, Waislamu wachache waliokuwa na silaha haba waliwashinda maadui zao waliokuwa wengi sana tena mahodari wa vita.

Hesabu ya Waislamu ilikuwa 313 hali maadui zao walikuwa elfu moja. Lakini kwa kudra ya Mwenyezi Mungu, mwenye uwezo wote, maadui wa Uislamu walishindwa vibaya sana na utabiri uliyotajwa hapo juu ukatimia barabara.

Pia ikumbukwe ya kwamba Kedar ni jina la mtoto mmoja wa Ismaili ambaye wazao wake waliishi katika sehemu ya Hijaz ulipo mji wa Makka. Wataalamu wa historia wamethibitisha kuwa Makureshi wa Makka (ambao ndio wale waliopeleka jeshi Madina kwenda kuwasaga Waislamu, lakini badala yake wakasagwa wao) walitokana na hao wazao wa Kedar. Na kule kushindwa kwao baada ya mwaka mmoja baada ya Mtume (s.a.w.) kuhamia Madina kunakamilisha utabiri huu wa Isaya bila upungufu wo wote.


5.     Ile aya ya mwisho, yaani 17, inatabiri ushindi wa Mtume (s.a.w.) juu ya maadui zake katika hivyo vita vilivyotokea mwaka mmoja baada ya Mtume kuhamia Madina. Kwa jumla utabiri huu mzima hauna uhusiano wo wote na Nabii mwingine ila tu Nabii Muhammad (s.a.w.) Wala hapana ushahidi wa historia unaoweza kutufanya tuseme ya kwamba pana Mtume mwingine aliyehama mji wake kwa ajili ya maadui zake na kisha akawashinda hao hao baada ya mwaka mmoja. Hayo yote yalitokea kwa Mtume wetu mtukufu Muhammad (s.a. w.) pekee.

Comments