UCHAMBUZI WA HOTUBA YA SHEIKH UWESU KATIKA MAZISHI YA
DOCTOR KABOUR.
Wiki hii tulimpoteza kiongozi maarufu wa
mkoa wa Kigoma, na Tanzania kwa ujumla, hususan kwa upande wa CHADEMA NA C.C.M.
Dr Kabour alikuwa mbunge wa kwanza wa
upinzani Tanzania nzima kuingia bungeni kwa tiketi ya chama cha upinzani (CHADEMA).
Yeye aliingia bungeni kabla ya uchaguzi mkuu uliohusisha vyama vingi vya siasa
mwaka 1995. Hii ilitokana na uchaguzi mdogo uliofanyika Manispaa ya kigoma
Ujiji baada ya kumpoteza mbunge wake wa kipindi hicho, marehemu Rajabu Mbano.
Dr. Kabour aliwahi kuwa makamu
mwenyekiti wa CHADEMA taifa, mbunge wa
Afrika na mwenyekiti wa CCM wa mkoa wa Kigoma. Alifariki wiki hii alipokuwa
akipatiwa matibabu katika hospitali ya taifa Muhimbili na kusafirishwa hadi
kigoma na kuzikwa Ujiji siku ya Ijumaa iliyopita.
Tunamwomba Allah amsamehe, na kumwingiza
katika rehema zake. (Sote tuitike Ameen).
Sheikh Uwezo Khalifan Kiumbe anasema,
kumekuwepo na mijadala katika vijiwe, hususani vya kahawa kujadili uhalali wa
sisi kumsafirisha Marehemu Kabour kutoka Dar Es Salaam mpaka Kigoma umbali wa
zaidi ya kilometa elfu moja, wakati Mtume alituagiza Mtu azikwe mahali
alipofia.
Akilitetea tendo lao hilo anasema kuwa
walimsafirisha marehemu kwa sababu huo ndio ulikuwa wosia wake, yaani azikwe
Ujiji, na kaburi lake lijengewe baada ya siku saba tokea kuzikwa.
Akaendelea kusema kuwa katika Uislamu
wosia ni muhimu uzingatiwe. Na hilo sio geni kutekeleza wosia ulioachwa na
Marehemu. Kisha akatoa mfano wa wosia waliowahi kuutekelezwa na masahaba wa
Mtume (s.a.w).
Akasema kuwa Bibi Fatuma bint Rasulillah
(s.a.w) alikufa akiwa hawaridhii mabwana wawili Abubakar na Omar. Fatuma ndio
mtoto pekee aliyeachwa na Mtume pindi alipofariki. Ieleweke kuwa Mtume anasema
kuwa Fatuma (a.s) ni mwanamke wa kwanza kuingia peponi. Hivyo jambo alilofanya
haliwezi kuwa nje ya Uislamu.
Baada ya baba yake (Mtume) kufariki, na
Abubakar kuchukua ukhalifa, alikwenda kwa Abubakar kudai mirathi yake. Abubakar
akadai kuwa alimsikia Mtume akisema kuwa mitume hawarithiwi. Ikabidi Fatuma
akose mirathi yake na hapo akamchukia sana Abubakar.
Siku chache baadaye bibi huyu akafariki
na kuacha wosia kuwa mabwana wawili Abubakar na Umar wasihudhurie mazishi yake.
Hili lilitekelezwa na mabwana hao hawakuhudhuria mazishi yake. Huu ni mfano wa
utekelezaji wa wosia wa marehemu tena uliofanywa na watu wema.
Kwa bahati mbaya hakueleza sababu za
bibi huyu mtukufu kumchukia Omar. Lakini kwa wachunguzi wa mambo wanafahamu. Ukweli
ni kuwa ukhalifa wa Abubakar ulitokana na Omar kuwalazimisha watu wamtii
Abubakar, kiasi kwamba alikwenda nyumbani kwa bibi huyu mara nyingi na
kuwalazimisha waislamu waliokuwa wakijua kuwa khalifa wa kwanza ni imam Ally (a.s)
wabadili misimamo na hivyo kumtii Abubakar kama khalifa wa kwanza.
Katika pilika pilika hizi, alifikia
mahala kupiga ngumi mlango wa bibi huyu na yeye akiwa nyuma yake, hapo mlango
ukampiga tumboni na kupelekea kupoteza ujauzito aliokuwa nao, ndipo akaugulia
kipigo hiki na miezi miwili baadaye akafariki dunia. Hivyo alimchukia Omar kwa
sababu ndiye aliyekuwa sababu ya kifo chake.
Ikumbukwe kuwa Uwesu huyu ndiye yule
yule aliyesimama majukwaani na kudai kuwa mashia ni makafiri. Tulipomuuliza ukafiri
wetu akasema kuwa tunawatukana maswahaba. Tulipomwambia tukisemacho ni historia
iliyomo katika vitabu vya Ahlul Sunnah alidai kuwa ni mashia ndio
waliozipachika historia hizo katika vitabu vyao.
Lakini leo anakuja na maelezo yale yale
ambayo yanaponukuliwa na Mashia, wao huchachamaa na kudai kuwa mashia wanawatukana
masahaba.
Hoja zangu ni hizi:
1. Nani alikuwa kwenye haki kati ya
bibi Fatuma na Abubakar katika suala la mirathi?
2. Je mtu mtakatifu kama Fatuma
anaweza kwenda kudai mali zisizokuwa halali yake? Na bado awe mtu wa peponi?
3. Qur’an inasema kila mtu
anarithiwa, je mitume hawakuwa watu?
4. Qur’an inasema kuwa Seleman
alimrithi Daudi, je Daudi hakuwa mtume? Mbona alirithiwa na Seleman?
5. Je aliyedhulumu na aliyedhulumiwa,
wote kwa pamoja wamo katika haki? Fikiri kiundani.
6. Wakati akitutukana mashia kwamba
hoja zetu zinawatukana maswahaba, je Uwesu hakuwa amevisoma vitabu vya historia
na kuuona ukweli huo? Je sasa ndio ameuona ukweli? Kama ameujua ukweli
hatutegemea achukie pale tutakapo hadithia historia za masahaba waovu na
madhalimu.
7. Au alikuwa akiujua lakini alikuwa
akiuficha ukweli? Kama alikuwa akiuficha ukweli basi atakuwa ni mnafiki na
wafuasi wake pia ni wanafiki.
Comments
Post a Comment