UTABIRI WA KWANZA WA MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W) NDANI YA BIBLIA

UTABIRI WA KWANZA WA MTUME MUHAMMAD (S.A.W.W) NDANI YA BIBLIA

Siku ya mkutano katika Horeb, wana wa Israeli walipokataa kusikia sauti ya Mwenyezi Mungu. Mungu alimwambia Musa. "Wametenda vema kusema walivyosema, mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao mfano wako wewe, nami nitatia maneno yangu kinywani mwake. naye atawaambia yote nitakayomwamuru. "Hata itakuwa, mtu asiyeyasikiliza maneno yangu atakayoyasema yule kwa jina langu, atauawa. Lakini nabii atakayenena neno kwa kujikinai kwa jina langu, ambalo sikumwagiza kulinena, au atakayenena kwa jina la miungu wengine, nabii yule atakufa." (Kumbukumbu la Torati 18.16-20).

Utabiri huu mtukufu unaonyesha mambo haya yafuatayo.
(i) Wana wa Israeli hawatasikia tena sauti yenye nguvu ya Mwenyezi Mungu.
(ii) Anayebashiriwa kufika ni Nabii.
(ill) Ataondokeshwa miongoni mwa ndugu wa Waisraeli.
(iv) Atakuwa mfano wa Musa.
(v) Maneno atakayoyasema yatakuwa ufunuo wa Mungu.
(vi) Atawaambia yote atakayoambiwa na Mungu.
(vii) Atanena hayo kwa jina la Mungu.
(viii) Asiyetaka kusikia maneno hayo ataadhibiwa.
(ix) Nabii wa uwongo atakayesingizia kutumwa na Mungu
atauawa.
(x) Atakayesema kwa jina la miungu wengine atauawa.

Sasa ni watu wawili wanaosemwa kuwa wametabiriwa katika Utabiri huu. Wakristo wanasema ni Yesu, na Waislamu tunasema ni Muhammad (s.a.w.w). utabiri wenyewe hautaji jina la mtu ye yote, ila tu imeeleza alama kumi za Nabii huyo.

Basi tuzichunguze alama hizo zinamwangukia nani katika manabii hawa wawili.
(i) Katika utabiri huu Waisraeli wanaambiwa kwamba hawatasikia tena sauti ya Mungu. Na inajulikana pote ya kuwa Yesu alikuwa Mwisraeli aliyezaliwa katika ukoo wa Daudi (Mathayo.
Mtume Muhammad (s.a.w.w) alikuwa Mwarabu. Hakuwa katika kizazi cha Waisraeli kilichonyimwa baraka za Mungu, kwa kukataa kwao kusikia sauti ya Mungu.

(ii) utabiri huu unasema huyo anayebashiriwa kufika ni nabii. Wakristo wanaamini ya kwamba Yesu alikuwa “Mungu-Mwana” au Mungu Mwenyewe, nao hawataki kabisa Yesu aitwe nabii. Lakini Mtume (s.a.w.w) aliitwa Rasuulullaahi (Mtume wa Mungu) na pia Nabiyyullaahi (Nabii wa Mungu).

(iii) lkumbukwe kwamba nabii Ibrahim - baba wa manabii – ndiye aliyemzaa Ismaeli na Isihaka. Wazao wa Ismaeli ndio Waarabu, na wazao wa Isihaka ndio Waisraeli. Mtume Muhammad (s.a.w.w) alitokana na Waismaeli ambao ni ndugu wa Waisraeli, kama inavyoagua bishara hiyo. Lakini Yesu mwenyewe ni Mwisraeli, wala hakutoka katika ndugu wa Waisraeli. Hivyo utabiri huu si wake.

(iv) utabiri unaeleza tena ya kuwa mtume huyo atakuwa mfano wa Musa. Nasi tunaona ya kuwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) ndiye anayeitwa mfano wa Musa katika Kurani tukufu (73:16). Yesu angewezaje kujifanya kama Musa hali mwenyewe alikuwa chini ya Sheria ya Musa? (Mathayo 5:17, 7:12, Marko 10:19. Matendo 24:14).

Hali ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) na ya Nabii Musa (a.s) zinafanana sana. Nabii Musa alizaliwa na wazazi wawili wala hakulaumiwa katika kuzaliwa kwake. Tena Musa alioa, alipewa Sheria mpya, alihama nchi yake baada ya kupewa utume, alipigana na adui zake, nao wakaangamia mbele ya macho yake, alikufa kifo cha kawaida, walitokea maimamu na mawalii katika umati wake, na mwishowe alikuja Masihi kusimamisha Sheria ya Musa.

Hayo yote yalipatikana kwa Mtume Muhammad (s.a.w.w) na hivyo
wamefanana kabisa. Sheria ya Mtume Muhammad itasimishwa tena hapa duniani pindi atakaporudi imam Mahdi (a.s). Lakini hakuna hata alama moja ya hizo inayopatikana katika dhati ya Yesu (a.s) sawa na itikadi za Wakristo.

(v) utabiri unaendelea kusema: “Nami nitatia maneno yangu kinywani mwake”. Yaani Mungu atamteremshia maneno yake.
Alama hii pia haionekani katika Yesu. Wakristo wanaamini ya kuwa Yesu alikuwa Mungu, kwa hivyo hakukuwa na haja ya kufunuliwa maneno kutoka kwa Mungu. Zaidi ya hayo, Kurani ndiyo Sheria ya pekee inayostahili kuitwa “Maneno ya Mungu”, maana haina hata neno moja lisilotoka kwa Mungu Mwenyezi.

(vi) Mtume (s.a.w.w) anaambiwa na Mwenyezi Mungu kufikisha yote aliyoteremshiwa (Kurani tukufu 5.68). Yesu (a.s) aliwaambia wanafunzi wake ya kuwa hatawaambia yote (Yohana 16.12-13). Hivyo utabiri huu haumhusu Yesu.

(vii) Alama ya saba pia haionekani katika Yesu. Mtu anayesoma Injili anajua ya kwamba Injili yote haina sura iliyoanza kwa jina la Mungu. Yesu anasema mara kwa mara. “Bali mimi nawaambieni” (Mathayo 5:22. 28, 34. 39. 44). Luka anasema, ameandika Injili yake kwa sababu. “Nimeona vema mimi nami kwa kuwa nimejitafutia usahihi wa mambo hayo yote tangu mwanzo, kukuandikia kwa taratibu, Theofile Mtukufu” (Luka 1:3-4). Hasemi kwamba alifunuliwa na Mungu, au ameongozwa na Roho Mtakatifu, wala hakuandika Injili hiyo ili watu wote waisome, bali alimwandikia mtu mmoja tu, Theofile. Paulo alisema. “Kwa habari za wanawali, sina amri ya Bwana. Lakini natoa shauri langu” (Wakorintho 7:25).

Ni dhahiri ya kwamba lnjili za leo ni mkusanyiko wa maneno ya watu mbali mbali. Lakini Kurani inataja jina la Mwenyezi Mungu katika mwanzo wa kila sura, na inaonekana Mungu alikusudia kutimiza alama hiyo wazi wazi. Tena Mtume (s.a.w.w) kabla ya kuanza kazi yo yote alikuwa anataja jina la Mwenyezi Mungu.

(viii) Waliokataa kusikiliza maneno ya Mungu yaliyotoka kinywani
mwa Mtume (s.a.w.w) na kuanzisha upinzani waliadhibiwa hapa hapa duniani. Vita vikali vilivyoangamiza maadui wa Uislamu vilikuwa adhabu ya Mwenyezi Mungu iliyoahidiwa katika utabiri huu, na bado kuna adhabu ya
akhera itakayowawakia walio maadui wa haki. Maadui kwa chuki zao za kukataa kuusikiliza ujumbe wa Mwenyezi Mungu walikusanya majeshi ili kuufutilia mbali Uislamu. Mwenyezi akawaamuru waislamu wajilinde. Wakapigana kwa msaada wa Allah wakawashinda maadui wao pamoja na kwamba waislamu walikuwa wachache tena wenye zana duni kabisa.

(ix) Wapinzani wa Uislamu wanasema ya kwamba Mtume (s.a.w.w)
alizua uwongo. Utabiri huu unawajibu na kusema mtu ye yote
atakayemzulia Mungu atauawa. Mtume (s.a.w.w) alikaa miaka mingi
duniani na akisha maliza kazi yake akafariki kifo cha kawaida.

Lakini Yesu je? Tukifuata imani ya Wakristo kuwa aliuawa msalabani, tunashurutishwa kusema ya kuwa (Mungu apishe mbali) alikuwa mwongo, maana bishara yasema kuwa nabii wa uwongo ndiye atauawa. Hivyo kufaulu kwa Mtume (s.a.w.w) na maendeleo ya kazi yake ni dalili zilizo wazi za ukweli wake.

(x) Bishara inaeleza tena ya kuwa mwenye kusema neno kwa jina la miungu wengine “Nabii yule atakufa”. Kwa kuwa Mtume (s.a.w.w) hakuuawa basi imethibitika ya kwamba yote aliyosema alifunuliwa na Mungu.


Muhammad wa aali Muhammad, swalawaatu

Comments

Post a Comment